JIPE RUKHSA
TUMEZOEA kupata hisia za fadhaa na za kujilaumu, tunapotenga muda, wa kujihudumia wenyewe au kufanya mapumziko japo ya nusu saa, ili kupumua, wakati tunaendelea na shughuli zetu za maisha.
Makuzi tuliopewa wanawake tokea utotoni, ni ya ‘utumishi’ kwa familia; jamaa; hata marafiki.
Tunaambiwa utotoni kwenye familia zetu kuwa “Mwanamke bora, ni yule anaejisahau yeye mwenyewe kabisa, na badala yake, kutunza wote waliomzunguka”.
Hii ni orodha ya baadhi ya salaa tunazopewa utotoni, ili tukue na misingi madhubuti ya kutimiza wajibu.
Hatuambiwi kuwa wajibu, lazima uandamane na haki.
■ Usiwe mvivu- hii inamaanisha hata kama unaumwa; au umechoka kupindukia; wewe, hautakiwi kupumzika.
Hivyo hivyo, ujisukume, wakija mawifi nyumbani bila taarifa, uingie jikoni kuwapikia; kuwatengea chakula; na baya zaidi, kusikiza masimango yao kwako.
Watakunyanyambua kuanzia mwili wako ulivyo, hadi nyumba ulivyoipamba.
Wengine watacheka “Ha Ha Ha!” huku wakikuangalia kwa kede na dharau.
Ukiwauliza wao, watoto wao wengine mateja; wengine wanakamkono; wengine watoro wa shule.
Na wao wenyewe kutwa kwenye msuto.
Lakini kwa vile walilipa mahari, ukaolewa, basi wanakufanyia kila aina ya tashtiti, mpaka unajiuliza “Nafanya nini humu kwenye familia hii? Ninako kwetu. Nikila na kushiba”.
Lakini mafundo tuliopewa tokea kuzaliwa, yanatufanya tuugue kimya kimya, na hatusemi kwa mtu masimango na kashfa tunazofanyiwa.
■ Ukubali kejeli kutoka kwa wanajamii, wengine ajnabi, hata hatufahamiani vizuri.
Waweza kutana na mwanamke mara moja tu maishani mwako, kwa muda usiozidi nusu saa, mukaamkiana.
Huyo akitoka hapo, atazunguka kwa simu; ana kwa ana; mpaka barua pepe; kukuchafulia staha; hadhi; heshima; utu wako.
Binafsi yamenipata.
Na wewe, hautakiwi kulalamika.
Unapilalamika, unaambiwa “Msamehe bure”.
Nimsamehe bure?
Hiyo lugha siielewi.
Unapokataa kusamehe, unaoneka mkorofi, asiye na maadili.
Zigo la lawama unatwishwa wewe.
■ Mwanaume anapokushika sehemu za mwili wako, na wewe ukimwambia “Stop It”, atakusema kwa wenzake-
“Yule kichaa”.
“Yule teja, avuta bangi”.
“Yule nishamwonja kingono”, jambo ambalo siyo kweli.
Unapolalamika kuwa huyu mwanaume alinitongoza nikamkataa, unaonekana wewe ndiyo mbaya, msungo.
■ Kwenye shughuli za wanawake kama arusi au vilio, kundi la wanawake wanaweza kukufumbia mafumbo.
Unatakiwa usirudishe mapigo. Unyamaze, umwachie Mungu, ile ya “geuza shavu la pili”.
■ Jirani anapotupa taka za matumbo ya kuku nje ya nyumba yako.
Hautakiwi kulalamika kwa Kamati ya Serikali ya Mtaa.
Au kutoa ripoti polisi.
Kumbuka “Mpende jirani yako, kama unavyojipenda mwenyewe” hata kama huyo jirani ni tumba ya mavi, haichukuliki.
■ Siku za mapumziko, ukiamua mchana upate kausingizi kadogo juu ya sofa, utasemwa na familia nzima.
“Mwangalie, alala kama pono”, kumbe wiki nzima ulifanya kazi za shuruba huko ulipoajiriwa; na nyumbani pia, ulifanya mapishi; ulifua; ulifanya repea nguo za watoto au za mume; nk.
Baada ya yote hayo, hautakiwi kupumzika, hata kwa nusu saa.
■ Unapokutana na watu, wakikuona tu, lazima wafanye gaslighting, ile ya kukudhalilisha.
“Umetisha na hiyo nguo”.
“Umenenepa kama mbuyu”.
“Mbona unaonekana hivyo? Waumwa? Umesawajika!” Ad nauseam.
Wewe, unaanza kujihami, na kujitetea, badala ya kumwambia “Eff Off”
■ Unapofanya shopping ya nguo, japo kitenge kimoja cha wax.
Nisikilizie maneno yatakayotoka “Mharibifu wa pesa”.
“Ushazeeka, nguo mpya ya nini?”
“Hiyo rangi ya kitenge haitokupendeza. Rangi yako kama papai”. 😩
Orodha ni ndefu mno.
Sasa, wakati umefika kwetu sisi wanawake, kusema “Sasa Basi. Imekithiri. Acha kunivunjia heshima na staha yangu”
Huu ndiyo wakati wa Kujipa Rukhsa
JIPE RUKHSA
● Kuwaambia mawifi wanaokuja nyumbani kukukejeli kuwa “Stop It”
● Kuwaambia wanaume wanaoshikashika mwili wako bila ridhaa yako to “Eff Off”
● Kujipa rukhsa ya kupumzika, iwapo mwili umechoka
● Kujipa rukhsa kujitunza; kujipamba; kujipenda
● Kujipa rukhsa kutumia pesa zako unavyoamua wewe mwenyewe
● Kujipa rukhsa ya kuwajibu gaslighters wanaokwambia “Mbona umenenepa kama mbuyu”
Uwajibu “Nimeridhia kunenepa. Ni mwili wangu. Sijakwambia unibebe, tumbili wewe”.
Jikaze utoe makombora ya majibu, la sivyo, kila siku utasiginwa kwenye jalala.
● Jipe rukhsa kuwaambia haters “I love myself”.
Akikasirika, mwambie akajinyonge kwa kamasi.
Tujadili
Together We Can Make it Happen
Leave a Reply