Je, wanawake Waswahili waliopigania Uhuru wa Taifa letu walikuwa washamba, hawakusoma?

Je, wanawake Waswahili waliopigania Uhuru wa Taifa letu walikuwa washamba, hawakusoma?

TUANZE kwa kuweka msisitizo kuwa wanawake Waswahili wakati wa mishe mishe za kupigania Uhuru hawakuwa:

 • washamba
 • mbumbumbu wasioweza kusoma wala kuandika
 • waliokuwa nyuma kimaendeleo

Ukweli ni huu:

 • Waswahili tokea makarne 7-9 nyuma, walishakuwa watanashati; jamii yenye utamaduni ulioendelea; na hawakuwa washamba, asilan
 • wanawake Waswahili walikuwa SIYO mbumbumbu, kwa sababu wakisoma na kuandika kwa ABJAD ya kiarabu.

Kutokufahamu kuandika na kusoma kwa ABJAD ya Kilatini, haikuwafanya wanawake Waswahili waliojitoa mhanga kugombea uhuru kuwa ni mbumbumbu.
Waliweza kusoma na kuandika kwa herufi za oriental/kiarabu.
Kipimo cha mtu kusoma siyo lazima aweze kutumia ABJAD ya wazungu.
Wachina; Wajapani; wa Bara Hindi; Wafarsi/Persian; walikuwa wanatumia ABJAD za kikwao, ambazo ni za zamani zaidi kuliko ABJAD ya Kilatini.
Tunawanyima heshima stahiki, kuwaita wanawake Waswahili waliojitokeza kugombea Uhuru kuwa walikuwa mbumbumbu.
Waliandika:

 • Barua
 • Tenzi
 • Orodha ya vitu
 • Ankara
 • Qasida
 • Nyimbo za taarab

Kwa herufi za ABJAD ya oriental, ambayo hapa kwetu inafahamika kama kiarabu, lakini ilikuwepo kabla ya Warabu kujikusanya na kuweka tamaduni zao.
Stadi ya kusoma na kuandika kwa herufi za ABJAD oriental, ililetwa Mwambao wa Afrika Mashariki, na Washirazi, kabla hata kuja wazungu kama Wareno, na kabla kuja Warabu.
Walikuja Washirazi kutoka eneo ambalo sasa lipo ndani ya nchi inayoitwa Iran, ambayo wakati huo ikitambulika kama Pars/Fars/Persian.
Hii ilikuwa kabla ya Ukristu na Uislam kuletwa huku kwetu.
Walikuja hao kutoka Fars, ambayo Waswahili wanaita Ajemi/Azmi, na walikuja na Imani ya Zorastrian.
Hadi leo, maeneo kama Tongoni; Kilwa; Mafia; Pemba; Rufiji; yapo magofu ya mimbar/sehemu ya kusali ya hao Zorastrian, ambao wakiweka moto kama sehemu ya ibada.
Hao, ndiyo walioleta tamaduni, zikachanganyika na tamaduni za Wabantu, ndiyo Waswahili ukazaliwa.

 • Kuvaa baibui ni ushamba?
  Inategemea unatoka ukanda upi, japokuwa siku hizi, madera na ukaya huvaliwa na wanawake wa kanda zote za Taifa
 • Kucheza ngoma ya lelemama ni ushamba?
  Kwangu mimi Mswahili, lelemama ni tunu ambayo tunaienzi na hatutaki ngoma ya lelemama ipotee
 • Wanawake Waswahili waliojitokeza kupigania Uhuru walikuwa wamezubaa?
  Hapana!
  Wangekuwa wamezubaa, TANU isingepata sapoti ya Waswahili, kwa sababu wanawake Waswahili walijitokeza kwa wingi, kuhamasisha wananchi wajiunge na mchakato wa kupata Uhuru
 • Uswahilini ndipo palipizaliwa vugu vugu ya kampeni ya kupata Uhuru wa Taifa, na wanawake Waswahili walikuwa chachu ya kusambaza kauli mbiu ya Uhuru; na ndiyo waliokuwa wanajitolea siyo tu kusimama kwenye majukwaa, bali pia walitumia mbinu hizi:
 • kupita majumbani kuhamasisha Uhuru na Umoja
 • kutunga nyimbo za lelemama zenye kuleta ari ya kuwa Taifa huru
 • kutumia fursa kama-
  > maulid
  > ngoma za mkole
  > arusi
  > vilio
  > hafla za taarab
  kuhamasisha wananchi, wanawake, kuwapa sapoti kwenye azma ya kupata Uhuru
 • kuchangisha fedha kutunisha Mfuko wa Uhuru
 • utamaduni; mila; desturi; za Waswahili, ni ukarimu, hivyo, wapigania Uhuru, hata waliotoka Bara, walikaribishwa kwenye hafla za Waswahili, ambazo zilikuwa fursa kusukuma gurudumu la Uhuru; na pia majumbani walikaribishwa, na kuwapa fursa ya kuwafahamu wamiji, ambao ndiyo hao, Waswahili
 • walitumia nyimbo ziluzokuwepo kwenye kauli mbiu kama ‘Hongera Mwanangu’; na walitunga tenzi na nyimbo makhsus, kwa ajili ya Uhuru
 • qasida zilitumiwa kuongelea Uhuru, na kuwa ni wajib kujitetea, kutoka kwenye utumwa, na kuwa huru, linalotokana na neno la kiarabu ‘Hur’ na ‘Huria’.

Wakati tunaadhimisha Miaka 60 ya Uhuru wa Taifa letu adhimu tuwakumbuke wanawake Waswahili waliojitolea kupigania Uhuru wa Taifa letu.
Tutakuwa tumewapunja, na hatuwatendei haki tusipowakumbuka.

Leila Sheikh
Dar es Salaam
December 7, 2021

 

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *