Mipaka kwa Watoto

Mipaka kwa Watoto

TUNAPOWEKEA watoto mipaka kwenye mienendo ya maisha yao, tunakuwa tunakiuka haki zao za maamuzi?
Au ni njia mojawapo ya kuwapatia watoto Muongozo juu ya:

• Maadili
• Heshima
• Kutojiingiza kwenye mambo ya kiutuzima, wakati bado ni watoto
• Ulinzi
• Mfumo wa maisha utakaowajenga

Wanaharakati tumegawana pande 3, tupo:

▪︎ Tunaoamini watoto wanahitaji Muongozo na Mafundisho ya Kiroho/Spiritual Guidance, ili wapate makuzi yatakayojenga binadamu wenye kuishi ndani ya misingi ya hicho, sisi tunakiona ndiyo uadilifu

▪︎ Wanaoamini watoto wapewe uhuru wa fikra na matendo, ili wakue kwa umadhubuti, na ukakamavu

▪︎ Wanaoamini watoto hata waliopo chini ya umri wa miaka 14, waruhusiwe kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi juu ya mustakabala na mwenendo, wa maisha yao

Uanaharakati siyo lazima tukubaliane juu ya kila suala, tunachofanya, ni kufata misingi tuliojiwekea, kwa kuzingatia Fungu la Haki za Msingi, kwenye Katiba ya JMT.

Tupo sisi tunaoamini kuwa Haki mojawapo ya watoto, ni kuwapatia msingi madhubuti wa elimu, na stadi za maisha; na kuwapa watoto Muongozo utakaowapatia Dira ya maisha yao.

Wapo wanaharakati wanaoamini Watoto wapatiwe fursa muhimu za maisha ya mafanikio, lakini tuwaachie wakue kwa uhuru, bila ya bughudha kutoka kwa watu wazima.

Na wapo wanaharakati wanaotaka Turudie maadili ya asili ili kuokoa kizazi cha sasa.

Wakati tunajadiliana njia ipi ni bora ya malezi ya watoto, (iwapo hiyo njia bora ipo); watoto wanaangalia filamu za kiutuzima kupitia smart phone; wanafundishana kuhusu vigodoro; wanaambiana “siyo lazima wasome, mbona Kaka Chibu (Diamond) na Kaka Konde Boy (Harmonize), wametajirika na kupata ustaa bila ya kusoma”.
Mtazamo huo unamshiko, kwa sababu ni kweli, wapo waliopata mafanikio bila kuvuka elimu ya msingi.
Na iwapo hawa manguli wangesoma chuo kikuu, labda wangesota, kutafuta ajira.
Lakini wamepata utajiri; umaarufu; tuzo kila aina; bila ya kuvuka elimu ya shule ya msingi.
Japokuwa tunasikia wameweka walimu kuwapa darsa muhimu ili waweze kufanya ushindani na mastaa kutoka mataifa mengine.

Wapi tunachora mstari kwa watoto, na kuwapatia Dira ya maisha, kuwa hata kama mimi sikusoma kufika chuo kikuu, nataka wanangu wafike huko.
Tuwawekee misingi madhubuti watoto mfano “Usijiingize kwenye ushoga, wa kugeuzwa mke, na wanaume wenzio!”
Au hapa tunawanyima watoto haki ya maamuzi juu ya miili yao?
Au tunawapa watoto Muongozo ambao tumewekewa kwenye Misahafu Takatifu?
Miongozo ya Mila na Tamaduni zetu za Kiafrika, amabazo kwa kiasi kikubwa, kimeweza kutuvusha kwenye bahari kuu ya maisha.

Je, uanaharakati inamaanisha tusiweke mipaka yoyote?
Tuwe huru kabisa, na tuongee kwenye majukwaa ya kijamii kuwa ‘Ndoa ni asasi iliyopitwa na wakati’.

Kujadili masuala haya ni muhimu, kama alivyoleta swali Mwalimu Vincensia, ambaye ni Mtetezi wa ulinzi wa watoto; ili tuweze kupata kianzio, na kupata mwanya kupigia debe umuhimu wa kutengeneza Sera ya Afya na Elimu na Stadi juu ya Miili ya Vijana ili wajitambue.

Binafsi, nishaitwa Kuwadi wa Mfumo Dume na mdada mmoja niliposema ‘Mwanamke kumpikia mumewe; kumtunza mumewe; kumheshimu mumewe; ni tunu 👋.

Kama hayo yananifanya niwe kuwadi wa mfumo dume, haya nimekubali.

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *