FEMICIDE- Mauaji ya wanawake

FEMICIDE- Mauaji ya wanawake

WANAWAKE wamekuwa wakiuawa duniani, kwa mikono ya wanaume, hususan, waume ndani ya ndoa; au wanauliwa na ‘wapenzi wao’ 🥺 japokuwa sisi watetezi wa ulinzi wa wanawake hatuwezi kuwaita ‘wapenzi’.
Ni wauaji wa kikatili, wanaotumia mabavu; vitisho; silaha walizokuwa nazo kama panga; magongo; au bastola, kuua wanawake kama njia ya kudhalilisha; kukomoa ‘jeuri’ ya wanawake; na kuonesha ubabe, kuwa anaweza kudunda mwanamke, na mara nyingine kuua mwanamke/wanawake, kwa sababu ‘anaweza’!
Jamii tumefumbia macho mauaji ya wanawake yanayofanywa na waume/’wapenzi’ kwa miaka mingi, na mara nyingi, kumlinda mhalifu wa mauaji, ili asipate adhabu ya kutumikia kifungo gerezani; au kunyongwa.
Kushiriki kwa jamii kwenye kuficha mauaji ya kikatili ya wanawake, kumesabibisha ukimya juu ya jinai hii ya mauaji ya wanawake.
Mwanaume atajihami, na familia na wanajamii kumlinda kwa kisingizio “Wivu. Mwanamke alikuwa kutwa nje, hashindi nyumbani”.
Hii ni kuhusu mwanamke anaefanya kazi nje ya nyumba, ya ajira au kujiajiri kama Mama Lishe, ili kuweza kukimu maisha ya familia.
Wanaume wengine wanaofanya jaribio la mauaji kwa kumpiga mwanamke nusu kufa, hutoa sababu kuwa ‘aliataka mwenyewe huyo mwanamke, kitu gani kilimsibu kuchelewa kurudi nyumbani? Kama uhaba wa usafiri, si angetembea kwa mguu?’
Hii ni kwa mwanamke anaetoka kliniki ya vipimo vya ujauzito.

Wapo wanawake waliouawa, na wanaoendelea kuuwawa, kwa kisingizio cha tuhuma za uchawi.
Hii hutokea pale mwanamke anapokuwa na eneo la shamba, la eneo la ujenzi wa nyumba, na yupo mtu au watu, wanaotaka kupokonya hilo eneo.
Njia rahisi ‘kuwaondoa’ wanawake ‘wakorofi’ wanaokataa kuachia maeneo au mali zao, ni kuwatuhumu uchawi ili hao wanawake wachomwe moto hadi kupata umauti.

Na wale wanawake wanaouawa kwa sababu ya kukataa ngono lazimishi.
Wengi wao hukodishiwa genge la wahalifu wanaume, na kumpiga mande, hadi umauti kumfikia huyo mwanamke.

Mauaji ya kikatili ya wanawake yanachukua taswira nyingi, na takriban mara nyingi zaidi, mauaji ya kikatili ya wanawake hufanywa na mtu, mwanaume, wanaemjua.
Femicide/mauaji ya wanawake yanaongezeka ulimwenguni.
Mataifa kama Brazil; Bara Hindi; Afrika Kusini; mauaji ya kikatili ya wanawake hufanyika kila kukicha.
Takwimu kutoka mataifa hayo zinatisha.
Huko mataifa ya Kiarabu, wanao mtindo wa kuua mabinti au dada, kwa kisingizio cha ‘mauaji ya kulinda staha na heshima ya familia/honour killing’, pale binti au dada anapofanya maamuzi juu ya maisha yake, ambayo yanakwenda kinyume na matakwa ya wanaume kwenye familia.

Hapa kwetu JMT Bara, takwimu za miaka 10 kati ya 1999-2009 zinaonesha ongezeko la mauaji ya wanawake kutokana na mazingira haya:

  • wivu ndani ya ndoa
  • binti au dada kukataa kuolewa na mume wa kuchaguliwa kwa ajili ya mahari, mauaji aina hii hufanywa na wanafamilia
  • mauaji ya wanawake wa umri mkubwa, kwa tuhuma za uchawi
  • mauaji ya wanawake wenye ulemavu wa ngozi/albino, kwa ajili ya matendo ya kishirikina
  • mauaji ya wanawake yanayofanywa na wakwe, baada ya mume kufariki, ili wanandugu wachukue mali

Ni mara chache, pale ambapo wahalifu wa jinai ya mauaji dhidi ya wanawake, hupata hukumu ya kunyongwa au kifungo cha maisha.
Wahalifu wa jinai hii mara nyingi ‘hulindwa’ na wanandugu na wanajamii.
Sasa, tunasema “Iwe mwisho wa mauaji ya kikatili ya wanawake na watoto wa kike”.
Kila tunapofumbia macho, au kumlinda mhalifu wa jinai ya mauaji, panatoa mwanya wenye tabia ya kutoa hasira yao kwa kutumia silaha, au nguvu za kimwili, waendelee na dhuluma hii.
Tunasema, sasa basi:

  • kuua wake/wapenzi kwa sababu eti ya wivu
  • kuua wanawake watu wazima kwa tuhuma za uchawi
  • kuua albino kwa sababu ya ushirikina
  • kuua binti, eti ameleta aibu kwenye familia, kwa kupata uja uzito kwenye umri mdogo

Kuua wanawake kwa sababu yoyote ile, tunasema “IWE MWISHO”.

Leila Sheikh
November 30, 2021

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *