Mwanamke Jithamini. Jiamini. Jipende

Mwanamke Jithamini. Jiamini. Jipende

TUKIFATA mrengo wa J 3 kwenye maisha yetu sisi wanawake,

• J- Jithamini
• J- Jiamini
• J- Jipende
tutakuwa tumepiga hatua kwenye maisha yetu, na kuweza kukabili changamoto za kujihisi sisi ni duni thamani- lacking in worth.
Ni ukweli usipingika kuwa tunavyojichukulia sisi wenyewe; tunavyojiweka kwenye kishubaka ndani ya jamii zetu; tunavyokubali kutungiwa lebo duni; ndivyo jamii inavyotuchukulia, na pia ndivyo jamii inavyotuweka kwenye kiboksi cha mtu/watu walio dhalili, na wasiostahili heshima; staha; na hadhi; kwenye jamii, na michanganyiko na wanajamii wenzetu.

Tabia ya wanawake wengi ya kujihisi wapo duni thamani, inajengwa na-

° Baadhi ya mila na tamaduni zetu, zile za kumweka mwanamke kwenye nafasi duni kabisa, ya kiumbe asiestahili heshima, wala huruma

° Malezi na makuzi tunayopata ndani ya familia zetu. Kila mara binti kukaripiwa, na kushushwa ari yake ya kujiamini

° Mfumo dume unaotawala sehemu nyingi za maisha ya binti/mwanamke, kuanzia ndani ya familia; shuleni na vyuoni; kwenye ndoa au mahusiano ya kimapenzi; sehemu ya ajira; na kwenye jamii zetu kwa ujumla

° Mabinti kutojengewa stadi za ukakamavu tokea utotoni; na kutojengewa uwezo wa kujilinda; na kutopewa ‘kongole’ wanapofanya vizuri kwenye mitihani shuleni, au kwenye ushindi wa riadha; kwaya; maulid; sanaa; nk.
Huu utamaduni upo, ambao umejijenga kwenye jamii zetu, kuwa “usimsifie sana binti, atapata kichwa na kiburi, hadi akienda ukweni baada ya kufunga ndoa, atakuwa jeuri”

° Bi arusi anapofundwa kabla ya kufunga ndoa kuwa ‘litakalomtokea huko anapoingia kwenye ndoa, asilalamike, ndiyo maisha sahih’, wakati alitakiwa aambiwe ‘usikubali kuonewa’

° Jinsi baadhi ya wanaume wanandoa wanavyokejeli wanandoa wenzao, mara nyingi mbele ya ndugu; jamaa; rafiki; wafanyakazi wa nyumbani; pia hujenga hisia za kuwa duni thamani kwa mwanamke

Huu mduru wa kupokonywa hadhi na utu wa mwanamke, unajenga mizizi kwenye fikra na hisia za mwanamke, na mara nyingine, mwanamke huweza kubali kufanyiwa udhalilishaji mpaka na wanandugu wa mume, na yeye mwanamke, kukubali hayo manyanyaso, kwa sababu ndivyo alivyofundwa.

Tabia hii, mwelekeo huu, unyonge huu, mara nyingi, mwanamke hurithisha binti wake, na kusukuma gurudumu la udhalilishaji, kizazi hadi kizazi.
Anapotokea mwanamke akainua sauti na kusema “Sitaki kudhalilishwa. Sikubali kuwa mnyonge. Shikeni adabu zenu, mimi SIYO kiumbe dhalili”, dah, inakuwa kama vile huyo mwanamke amevunja miiko yote ya kijamii.
Mwanamke huyo atarushiwa laana kutoka kwa wanajamii, mara nyingine, wakiwemo ndugu zake.
Mwanamke huyo atapewa kila aina ya lebo na majina-

• Kichaa
• Mvuta bangi
• Msungo
• Balanzi
• Mkosa sera na dira
• Amevamiwa na mapepo mabaya
• Pili pili kichaa
• Varu varu/frustrated
• Hajapata mtu wa kumkomesha
• Msagaji
• Mchawi, mwanga
• Kakosa aibu hata ya kuombea maji ya kunywa
• Hana mipaka wala ashaakum
orodha ni ndefu.

Yote hata, kwa sababu mwanamke ameweza kuthubutu kuchora mipaka kwa watu waliomzunguka; kwa kukataa Kudhalilishwa; kwa kusema “Stop it!”.
Bahati mbaya, wanawake wengine wanakuwemo kwenye mkumbo huo wa udhalilishaji wa wanawake wenzao.
Hata kama wao hupata changamoto ya kuchukuliwa kuwa ni duni thamani, hawaachi ‘fursa’ ya kumkebehi, na ya kumdhalilisha mwanamke mwenzao.
Hii huleta simazi; majonzi; hisia za kutojiamini; kwa muathirika.
Wakati huo, gurudumu la ukandamizaji linaendelea kusukumwa, kwa wanawake wengine kwenye jamii zetu.

Nini kifanyike?

▪︎ Tuanze kwa kutambua kuwa hili tatizo lipo kwenye jamii zetu

▪︎ Tutoe elimu jamii kupitia vyombo vya habari, hasa redio, inayowafikia wananchi wote, juu ya-
• mahusiano ya kifamilia, na nafasi na mchango wa mwanamke kwenye familia

• Malezi na makuzi ya watoto- wa kike na wa kiume. Binti asichukuliwe kuwa ni duni thamani

• Mitaala ya elimu iingize somo juu ya jinsia, na ujenzi wa ukakamavu kwa watoto wa kiume, na wa kike

• Viongozi wa dini waongelee umuhimu wa heshima kwa wanawake

• Mkole- mabinti wafundwe jinsi ya kuheshimu na kuijali miili yao, badala ya kufundwa ngoma za vigodoro

• Wakati wa arusi, kwenye Kitchen Party, bi arusi apewe darsa juu ya dhima, na haki na wajibu, ndani ya ndoa.
Hapa inabidi waitwe manyakanga aina nyingine, siyo wa manyago ya vigodoro, bali manyago ya haki za msingi kwa wanandoa wote wawili

• Wanawake wapatiwe warsha kupitia vipindi vya redio, kuwa wakakamavu.
Wasikubali hali ya kuwa duni thamani

Zaidi ya yote, iwapo mmoja wetu sisi wanawake, ameweza kujikwamua kutoka kwenye hali ya kuwa duni thamani, na kuweza kunyakua hadhi yake, na utu wake, tusimnyooshe kidole, na kumpachika lebo.
Tumchukulie kuwa ni Mshindi!
Hakuna anayejua kwa nini mwanamke anaamua kuondoka kutoka kwenye ndoa, ambapo wanawake wenzie wanaweza kumwonea gere.
Atoke kwenye utajiri wa mume, aondoke na kibegi kimoja, atafute sehemu ya kujibanza, ili aokoe afya ya hisia na afya ya akili.
Mwanamke wa aina hii anahitaji sapoti yetu.
Anahitaji heko.
Na awe mfano wa kuigwa.

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *