BODA BODA
HIKI CHOMBO chenye jina lenye maneno mawili, kimetukomboa kwenye suala la usafiri.
Siku hizi, wengi wetu hutumia chombo cha boda boda kama usafiri, na chombo hiki kimeturahisishia maisha, hususan, kwenye usafiri wetu, na wa mizigo yetu.
Hii ni kwenye majiji, hadi vijijini, boda boda imekuwa ‘mkombozi’.
Miaka ya nyuma kabla ujio wa boda boda, wengi wetu tukipanda dala dala, ambazo zikijaa na kufurika hadi nje ya mlango.
Isitoshe, tukisimama kwenye vituo vya dala dala kwa masaa, kungoja usafiri.
Boda boda zimetukomboa.
Tukienda vijijini kwetu, miaka ya nyuma tukishuka bara bara kubwa; afu twabeba mizigo yetu, Wabondei tunaita ‘bahasha’, neno bahasha (ya barua) imetokana na kifungia mzigo kwa lugha ya Kibantu); na kwenda vijijini kwetu kwa kutreki, mara nyingi, kwenye umbali mrefu, hadi kilometa 15, au zaidi.
Tukifika huko, tunakuwa hoi binti taabani.
Siku hizi, tukishuka kutoka bus, twapanda boda boda, na kuipandisha bahasha yetu kwenye boda nyengine, haooo, tunakata mbuga.
Tena nauli ya boda boda ni poa tu.
Tushaona sofa kubwa limefungwa na kamba, juu ya boda boda, linahamishwa.
Tushaona shehena ya bidhaa za dukani zimebebeshwa boda boda.
Tushaona abiria wamekaa mkao wa mshikaki juu ya boda boda, mara nyingine, hata abiria wanne.
Tushaona mwanamke mja mzito kashikwa na uchungu, apelekwa kliniki kwa boda boda, amefungwa na kanga ili asianguke, ndiyo seat belt.
Boda boda ni mkombozi.
Tatizo?
Pale ambapo hapazingatiwi yafuatayo:
▪︎ Boda boda likiwa bovu, breki haifanyi kazi, na badala ya kuipeleka kwenye matengenezo, boda boda inafanya kazi ya kubeba abiria, bila kujali usalama wa abiria; madereva wa vyombo vingine barabarani; na shehena wanazobeba.
▪︎ Dereva wa boda boda kupewa dhima juu ya uendeshaji na matunzo ya chombo cha boda boda, bila kupata mafunzo yoyote.
Tajiri, mmiliki wa boda boda, anampa chombo kijana aendeshe, na kila jioni, tajiri aletewe fungu lake la pato.
Hajali pametokea nini huko viwanja vya fisi kwenye utafutaji wa fedha, almuradi anapelekewa fungu lake.
▪︎ Kutokua na leseni kwa waendesha boda boda, na kibaya zaidi, wanapokamatwa na trafiki, kutoa kitu kidogo, na kuachiwa kuendesha boda boda bila leseni.
▪︎ Uvutaji bangi; unywaji pombe; mihadarati; miongoni mwa baadhi ya dereva wa boda boda, kumesababisha ajali nyingi mno!
Leo, jirani yangu, mdada mpika na muuza supu ya utumbo; mapupu; na makongoro; alikuwa amekaa kando kabisa ya barabara, na masufuria yake ya supu, kazolewa na boda boda, akagongwa kichwa vibaya mno.
Yupo hospital ya Mwananyamala, hali mbaya sana.
Dereva wa boda boda alikuwa anashindana na mwenzie, nani mtemi zaidi, ndiyo kupoteza kontro ya chombo, na kwenda kumzoa dada mpika supu, mwenye watoto 3 wanaomtegemea.
Mara nyingine, boda boda akiona wasichana, anafanya kama anawatishia, kwa kuwasogelea karibu kabisa.
Tushaona watoto wakigongwa na boda boda.
Wazee; walemavu; wenye biashara za urembo; wakigongwa na boda boda.
Utemi!
Inatukumbushia tuliowakabidhi dhima ya kusimamia masuala ya mustakabala wa Taifa letu adhimu.
Wanakuwa kama dereva wa boda boda.
Wakishika chombo, wanajiona wao ni wao.
Uwiiii…
Tujadili
Together We Can Make it Happen
Leave a Reply