Adha ya Ukatili wa Kijinsia
Picha kwa hisani ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania TAWLA
KILA mwaka ifikapo Novemba 25, wanaharakati na wadau, tunaanza kuadhimisha Siku 16 za Kupiga Vita ili Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia.
Mwaka huu 2021, tutakuwa tumetimiza miaka 30, tangu 1991, ambapo wanaharakati na wadau ulimwenguni, tulianza kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia, na umuhimu wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Kauli Mbiu mwaka huu 2021, ni Wanaume na vijana wa kiume, wanahitajika kwenye Kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Mwaka 1991, wakati AZAKI/Asasi za kiraia/AZAKI/civil society organisations CSOs, zilipokuwa bado changa, na pale ambapo wanaharakati wa JMT akina sisi, tulikuwa Dogo kabisa, tuliungana kwenye Shirikisho la kuadhimisha Siku 16 za kupiga vita ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, ambalo waliratibu WILDAF Tanzania.
TAMWA tulipokea dhima zifuatazo:
- Kusimamia utoaji na usambazaji habari juu ya matukio tutakayoadhimisha kwenye Siku 16, ili wanajamii wapate taarifa, na pia wajumuike nasi wanaharakati ili Kampeni iwe shirikishi
- Kuratibu ukusanyaji wa data za vifo/mauaji yatokanayo na ukatili wa kijinsia kutoka vituo vya polisi vya mikoa 5 JMT Bara; Msajili wa mashtaka ya jinai, hususan, mauaji ya wanawake yatokanayo na ukatili wa kijinsia majumbani; rekodi za Mahakama za Wilaya za mikoa 5, JMT Bara.
- Kuratibu Usiku wa Maombolezo juu ya wanawake waliopoteza maisha kutokana na ukatili wa kijinsia, hususan, majumbani, kwenye familia.
Tulivaa vilemba vyeusi na kushika mishumaa na kuomboleza vifo aina hiyo.
Tulitayarisha shuka/quilt tuliofuma majina ya wanawake, ambao wanafahamika, kwa kupata umauti kutokana na ukatili wa kijinsia.
Tuliuita Usiku wa Vibatari ambapo wanawake kwenye mikoa mingi wakiwasha mishumaa au vibatari, na kuwakumbuka wahanga waliopoteza maisha kutokana na ukatili wa kijinsia - kuandika makala maalum na kutayarisha vipindi maalum kama njia ya kuongeza uelewa kwa wanajamii, juu ya ukatili wa kijinsia
Ilipofika mwaka 1992, Levina Mukasa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliamua kuchukua maisha yake kwa kunywa vidonge vya chloroquine, baada ya kunyanyaswa kijinsia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Sisi TAMWA, na mwanachama Chemi che Mponda, tulifatilia hilo tukio.
Wakati huo, wanawake walishaanza kusikia kuhusu TAMWA, wakawa wanatufata ofisini pale Kisutu, na sisi tukamuua kuanzisha Kituo cha Msaada kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia yaani Crisis Centre.
Ikabidi tutafute sehemu nyingine ambapo patakuwa na faragha kwa ajili ya wahanga, na pia, pawepo nafasi ya kutosha kwa utoaji ushauri nasaha na msaada wa kisheria.
TAMWA tuliandika kwa
- Msajili wa AZAKI
- Idara ya Ustawi Jamii
- Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
- Ofisi ya DCI
Kuomba kibali cha kuendesha Kituo cha Msaada kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, Crisis Centre
Kwa bahati nzuri, tulipata sapoti kutoka wahusika wote.
Aidha, tulipata sapoti kutoka kwa wanajamii.
- Wapo waliojitolea wenyewe kuja kusaidia kwenye Kituo, bila malipo
- waliotoa msaada wa sukari; majani ya chai; vikombe nk ili wahanga wa ukatili wa kijinsia wanapokuja kupata msaada, tuweze kuwahudumia
- waliotoa nguo na sabuni ya kuoga na maziwa ya unga kwa ajili ya watoto, ambao msaada ulisaidia wahanga
Misaada ilikuwa mingi, naorodhesha baadhi ya wanajamii waliojali, na kutoa msaada
- Hayati Mzee Reginald Mengi, na Hayati Mama Mercy Mengi
- Hayati Mzee Alnoor Kassam na Hayati Mama Yasmin Kassam
- Hayati Mzee wangu, Col Abdulkarim Sheikh, alietuazima gari ya pick up, tuweze kufanya kazi ya wito kwa ufanisi
- Mhe Said Bakhressa, alietoa chakula tupeleke kwenye Kituo cha Wazee, Kolandoto.
Tulianzisha Kituo kwa wazee wanaotuhumiwa uchawi, na wengine kuuwawa.
- Serikali ya JMT Bara, Mkoa Shinyanga, na Hayati RC Mzee Babu, ilitupatia Kituo cha Kolandoto, kuwapa hifadhi wazee wanaotuhumiwa uchawi, na maisha yao kuwa hatarini
- Shirika la Reli Tanzania, walisafirisha chakula na vifaa vingine kutoka Dar es Salaam, kupeleka Shinyanga, kwa ajili ya Kituo cha Kolandoto. Shirika la Reli Tanzania lilijumuika nasi kwenye Kampeni
- Hayati Ali Mufuruki na W Store, kwa kuchangia nguo nk kwa ajili ya wahanga wa ukatili wa kijinsia
- Hayati Mhe Bakari Mwapachu, kwa kuwepo na sisi bega kwa bega
- Jeshi la Polisi kwa kusaidia kuwakamatat washutumiwa, na kusimamia kesi mahakamani
- Clouds Media, hususan Bro Joseph Kusaga
- Channel Ten
- Habari Corporation, Chief Jenerali Ulimwengu na Chief Bwire, kwa kutupatia msaada
- The Daily News
- Magazeti ya Uhuru na Mzalendo
- Radio Tanzania
- Radio Zanzibar
- Hayati Richard Nyaulawa, wa Business Times Ltd
- Chief Joyce Mhaville wa ITV
- Hayati Charles Chipungahelo (Chips)
- Hayati Mama Anna Idrissou
- Chief Sarah Luhindi
Orodha ni ndefu.
Tunapoadhimisha Miaka 30 ya Kampeni ya Siku 16 za kupiga vita ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto hatuna budi kuwapa shukrani waliojitolea kwenye Kampeni.
Na shukran, hongera, hai hai (pole kwa Kibondei) kwa wanaharakati wote waliojitoa mhanga, ili Taifa letu adhimu liweze kuishi bila ya ukatili wa kijinsia.
Bado safari ni ndefu.
Wengine 😟 tumetumia usichana wetu kwenye utetezi, hata tukisahau kuchana nywele, lakini tumepiga hatua.
JMT bila ya ukatili wa kijinsia INAWEZEKANA, iwapo sote kwa pamoja, tunaamua kuingia ulingoni.
Leila Sheikh
Tanga,
Novemba 24, 2021
Leave a Reply