MAONI

■ Wananchi tupatiwe elimu jamii juu ya maana na utekelezaji wa Criminal Justice/Haki kwenye Jinai.
Hii ifanyike kupitia vyombo vya habari, hususan redio, ambayo ni chombo cha habari shirikishi, na kinawafikia 89%-93% ya walengwa; hata waliopo kwenye vitongoji ambavyo vipo kidogo na umbali.

■ Pawepo na Daftari la waliokutwa na hatia ya jinai ya unajisi wa watoto; na wakatumikia adhabu ya kifungo, ambacho Marekani huita ‘Correctional Centres/Vituo vya Kurekebisha Mwenendo wa Wajinai’.
Daftari hili liwe na maelezo ya hao waliokutwa na hatia ya unajisi wa watoto kama-

▪︎ Jina
▪︎ Picha
▪︎ na alama nyingine
Hii ni kwa ajili ya ulinzi wa watoto.
Takriban mara nyingi, waliofanya unajisi wa watoto, huwa wanarudia kutenda jinai hiyo wakirudi kwenye jamii.
Wananchi tunataka Haki ya kupewa taarifa kuwa miongoni mwetu, yupo mtu alietenda jinai ya unajisi wa watoto; akatumikia adhabu; na kuwa sasa anaishi miongoni mwetu.

■ Taifa liwekeze zaidi kwenye kuzuia uhalifu wa jinai, na siyo tungoje uhalifu wa jinai utendeke, ndiyo tuchukue hatua.
Kwenye hili, elimu jamii ni muhimu mno, hasa kupitia nyenzo ya redio, kuwafikia wananchi.
Elimu jamii itoe uelewa juu ya makosa ya jinai; adhabu ya makosa ya jinai iwapo mtuhumiwa atakutwa na hatia; na jinsi gani sisi wananchi tunaweza kusaidia vyombo vya usalama na ulinzi, ili tupunguze matukio ya makosa ya jinai.

■ Dawati la Jinsia liwepo kwenye-

▪︎ Vituo vya Polisi
▪︎ Sehemu za ajira ya rasmi na isiyo rasmi
▪︎ Kwenye Vyuo vya elimu
▪︎ Penye mikusanyiko ya watu, mfano gulio
▪︎ Shule za msingi na sekondari ili kusaidia watoto wasinajisiwe

■ Tuainishe kwa lugha nyepesi na rafiki, aina ya makosa ya jinai.

■ Pawepo na wakalimani wa lugha ya ishara kwenye mlolongo wa kutafuta haki kwa watu wenye ulemavu wa kusikia na kuongea.

■ Serikali za Mtaa zipatiwe nyenzo na uelewa juu ya jinai ya vurugu za majumbani, ziweze kutoa msaada kwa muathirika kwa maelezo, ili afate mlolongo wa kudai haki.

■ Tupitie upya sheria kadha ili kuzirekebisha iwapo zina mapungufu.

■ Wanawake waliopo gerezani wapate haki ya kuvaa hijaab/kufunika kichwa.
Hii ni haki ya binadamu, kuweza kufunika ukaya kichwani.
Wanawake waliopo rumande au gerezani, mara nyingi hawaruhusiwi kuweka hijaab, hadi mwaka 2018, sisi Women Matters Forum WMF, tulipodai haki hiyo kwa wanawake wanaotaka kuvaa hijaab/ukaya kichwani.

■ Ulinzi kwa wanawake waliopo rumande au gerezani.
Tumeshaona baadhi wanapata ujauzito.
Inatufikirisha wanaharakati kuwa lazima palitokea ubakaji huko.

■ Vyombo vya habari vipewe Warsha juu ya kutoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu wa jinai.
Wanahabari wengi, wa YouTube channels huwa wanatoa hukumu kwa mtuhumiwa, kabla hata malalamishi kusikizwa mahakamani.

Together, we can make it happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *