Ingekuwaje iwapo TAMWA tusingemtoa Bibi Titi Mohamed arudi kwenye medani ya uanaharakati?

Ingekuwaje iwapo TAMWA tusingemtoa Bibi Titi Mohamed arudi kwenye medani ya uanaharakati?

Ingekuwaje iwapo TAMWA tusingemtoa Bibi Titi Mohamed arudi kwenye medani ya uanaharakati?

NAKUMBUKA mwaka 1992, Da Maria Shaba (Da Ma) aliponiambia “twende kumwamkua Bibi Titi Mohamed”.

Nilibaki mdomo wazi.
“Bibi Titi Mohamed, Da Ma?”
“Ndiyo huyo” akajibu Da Ma.
Hapo ndipo nilipokwenda nyumbani kwa Bibi Titi Mohamed, Upanga, Dar es Salaam na kuanza urafiki naye.
Nikimwita ‘shosti’.
Baadaye, wana TAMWA akina
• Mama Eda Sanga
• Zaynab Vulu
• Pili Mtambalike
• Marehemu Tabu Ndziku
• Mama Deborah Mwenda
Tukapeleka hoja Mkutano Mkuu wa TAMWA, AGM, ndiyo Bibi Titi Mohamed akaombwa kuwa Mlezi wa TAMWA.

Wapo waliotuambia “Mhaini huyo, alifanya madhambi ya kutaka kuleta vurugu kwenye Taifa”.

Sisi, tukawajibu

Kwetu, Bibi Titi Mohamed ni mwanaharakati wa kupigania Uhuru wa Taifa letu adhimu, na ameweka njia ili sisi, tuwe kwenye medani ya harakati za ukombozi wa wanawake na utetezi wa wanawake kupata fursa

Tulikuwa naye Bibi Titi Mohamed, hadi siku alipopimzishwa mwaka 2000.
Kila hafla ya TAMWA, Bibi alikuwepo. Akituita tumchagulie dera na mtandio wa kuvaa kwenye hafla.

Tulianza kumhoji juu ya maisha yake kuanzia 1997-2000.
Bibi alikuwa mchangamfu, na muwazi.

Kwenye huu mwezi mmoja, tunaona watu wanafumka, wengi wakidai ‘wao ndiyo waliomuenzi Bibi Titi Mohamed’.
Haya, asaa kheir.

Nimehojiwa na CHANZO TV kuhusu kipande kidogo cha maisha ya Bibi Titi Mohamed, na nini sisi wanaharakati tungependa kifanyike?

Jibu langu?

● Tupatiwe Bibi Titi Mohamed Day, November 11, siku alipopumzishwa

● Tupatiwe Makumbusho ya Wanawake ambapo hapo tutaweza kuweka kumbukumbu za wanawake jasiri wa Taifa letu adhimu kuanzia Bibi Titi Mohamed na Mama Maria Nyerere, na Mama Sofia Kawawa, kuendelea kwa akina Mama Lucy Lameck na Mama Salome Kisusi na Mama Thecla Mchauru.
Mpaka akina Mama Gertrude Mongella; Mama Leah Lupembe; Mama Teresa Ntare; Mama Anna Makinda; Mama Anna Mkapa; Mama Tatu Nuru; Maj General Zawadi Madawili; Mama Maria Kamm nk.
Hawa na wengine ndiyo waliotuwezesha sisi kuthubutu kwenda Dodoma, kukabiliana na Wabunge mwaka 1997, na TZS 600,000 tu mfukoni, tutakaa kwenye mahema, tukaletewa mikate na maharage kutoka kwa Wasamaria, ili tuweze kupata Sheria ya Makosa ya Kujamiiana SOSPA 1998.
Bila ya wao kuacha alama za nyayo na sisi kuzifata, labda tusingepata uthubutu!

● Tupatiwe ufadhili – Special Fund- ili tusiombe fedha kutoka kwa wazungu tuweze kuweka kumbukumbu ya historia za wanawake waliochonga njia, na sisi, akina Leila, tukaweza kuthubutu.

La ziada, tukumbuke Masimba Jike walikuwa wengi.
Mama Maria Nyerere, kwa kutoa sapoti kwa Kambarage, ndipo Kambarage akaweza kuacha kazi ya ualimu Pugu Sekondari, akaingia kwenye harakati za ukombozi wa Taifa.

Akina Bibi Mluguru waliochangia nasaha; pesa; na chakula; kuwawezesha vijana waingie kwenye Ulingo wa Harakati za Kupigania Uhuru.

Tuwaenzi.
Tuwape stahiki yao kama wanaharakati.
Tuweke kumbukumbu ya historia zao.

Labda ipo siku, miaka 50 kutoka leo, watainuka vijana kutuenzi sisi.

Leila Sheikh

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *