MJANE

NENO MJANE likitajwa kwenye jamii zetu, taswira inayotujia ni ya mwanamke ambaye amefupisha maisha ya mumewe.
Mwanamke balanzi.
Mwanamke nuksi.
Kwa nini asife yeye?
Hivi, ndivyo jamii zetu zilipojikita- kuwa mjane anakuwa hana thamani tena; na inawezekana yeye, ndiye aliemuua mume.
Tunasahau kuwa yeye, ni miongoni mwa waathirika wakuu, pale mume anapofariki, waathirika wakiwemo na watoto; na wazazi wa huyo mume.
Kufiwa na mume hapa kwetu inachukuliwa kuwa ni nuksi kubwa, na yapo makabila ambayo hayaruhusu mjane kuhudhuria arusi, au hata sherehe nyingine, kwa kisingizio, ataleta nuksi.
Mjane, anageuka kiumbe dhalili; nuksi; mkosi; balanzi; mla mume.

Inapokuja kwenye usimamizi wa mirathi, hata kama mjane amechangia ujenzi wa nyumba; au kuwekeza kwenye shamba, au kwenye biashara; mfumo dume hupelekea wakwe na wanajamii kuchukulia hiyo mali yote ni ya marehemu.
Ndugu wa marehemu mume wanaweza hata kumfukuza mjane kutoka kwenye nyumba ya ndoa, eti arudi kwao, ambapo aliaga huko baada ya kuolewa, miaka 40 nyuma.

Mjane anaweza kulazimishwa kuolewa na shemeji, hata kama hataki.
Mila ndivyo inavyotaka, ili mali isiende njoo ya ukoo.

Mjane anawekwa chumba cha uani, na mashemeji, hukaa starehe, kwenye nyumba nzuri, ambayo mjane alichangia kujengwa.
Mjane, hana ruhusa kucheka; kujipamba; kufurahia maisha.
Ataitwa mchawi, kamuua mume.

Mume, akifiwa na mke, kabla kaburi halijatulia, atafutiwa mke, haraka!

Nini Kifanyike?

■ Sheria ya Mirathi ipitiwe upya, na vipengele viongezwe, ili masuala ya mirathi yapewe kipaumbele mahakamani

■ Wananchi wapatiwe elimu jamii juu ya umuhimu wa kuacha wosia juu ya mali

■ Elimu jamii ni muhimu kuhusu magonjwa ya kuambukiza, kwenye kurithi wajane

■ Jamii zetu ziambiwe ‘Kifo ni faradhi, siyo balanzi, hivyo tuache kulaumu wajane mume anapotangulia mbele ya haki’

■ Tabia ya kunyanyasa wajane itengenezewe Sheria, ili wajane wasiteswe

 

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *