Choko Choko Mchokoe Pweza
WASWAHILI huwa tunapenda ‘misemo’, siyo tu wakati wa maongezi na wenzetu, bali hata kwenye:
▪︎ Kanga– huwa tunaweka usemi wa mafumbo; au wakutoa salaa; au wa kusherehekea sikukuu kama Eid; au kuomba radhi; kumshukuru Mwenyenzi Mungu; na zaidi ya yote, kurusha makombora ya majibu kwa mahasimu wetu, ambao wametutendea ubaya.
Wengi hujiuliza, hasa watu wa sehemu za Bara, “Hii misemo, au maandishi kwenye kanga, wanaitoa wapi watengenezaji wa kanga?”
Ukweli ni huu- wanatoa kwenye nyimbo; mashairi na tenzi; qasida; na mara nyingi, wanawake, makhallat, hupeleka ‘msemo’ kwa muuza kanga kwa wingi, naye hupeleka huo usemi au jumbe, kwa watengenezaji wa kanga wa hapa JMT; Bara Hindi; au Indonesia.
Kanga ni njia muhimu mno kwenye mawasiliano yetu wanawake wa Kiswahili.
Binafsi nilishavaa kanga yenye usemi “Si Kizizi, ni Bahati Yangu”.
Nilituma ujumbe kwa mwanfulani. Akaupata.
Mara nyingine tena nilivaa kanga kwenye walima ya arusi yenye fumbo “Mumeo akome kunifatafata”.
Hadi raha.
Tatizo la Mswahili, usimtoneshe jipu na kucheka, wakati wewe unalo donda ladoda usaha.
Mswahili lazima atachukua bizari na pili pili kichaa, apake kwenye hilo donda.
Ataongezea ukwaju na halidi.
Afu, atachukua jiti lilofungwa tambara bovu, atumie kama kijiko cha kupaka misalo kwenye donda.
Jamani huwa nasema “Usimchokoze Mswahili, waweza kulia machozi ya damu”; hasa unapoanza wewe uchokozi.
Kiswahili na vidokezo vyake kilizaliwa kwetu; kikajavunja ungo wakati wa mishe mishe za kugombea Uhuru wa Taifa.
Sasa, Kiswahili kinageuzwa kuwa kilugha- hakuna herufi ya H.
Sikubali!
Lazima niseme “Hallo ya Tanga”.
Makhallat wa Tanga au Zanzibar hujibu “Nasukuma bembea, naona tamu eenh.. “
▪︎ Tenzi– Waswahili tumejaaliwa ujuzi wa kutunga tenzi, hata beti 1,000, kupeleka ujumbe kwa mahabuba wetu, tumfurahishe.
Kwa mahasimu, twaweza tunga tenzi za beti 5,000, tukamnyanyambua mtu, hadi atamani kujificha.
Watu dizaini hii ni wale, ambao hutumia madaraka waliokabidhiwa kukandamiza watu, hasa anapokuwa na ajenda binafsi.
Inakuwa siyo sehemu ya kibarua chake, bali ajenda binafsi ili apate uradi wake.
Watu aina hii khatari sana na Mwenyenzi Mungu amewawekea sehemu yao huko jahanam.
Mtu aina hii yupo tayari kufanya lolote, hata ikibidi watu wagombane hadi kufikia kuua; ili uradi wake, niseme ulafi wake wa kupata madaraka, utimie.
Watu aina hii huweza hata kununua kidole cha albino ‘Audhubillahi min dhaalika’, ili nyiradi zake zitimie.
Sasa, akipata kichochezo cha utunzi, siyo utenzi, wa taarifa ya uongo; dah, nisikilizie atakavyoruka ruka.
Aweza hata kucheza sunsumia, kwa furaha.
Kapata kisibo cha kujambia ati, si lazima afurahi.
Ndiyo huingia ulingoni, kuleta uchafuzi.
Uongo; mifaraka; istizai; choko choko; peke peke; fata’ani; vyote hivyo na zaidi, ni silaha zake kwenye vita ya kutimiza uradi wake.
Siku nyingi aliweka azma apande ghorfa ya vyeo hadi afike juu.
Anahitaji mkongojo kupanda ghorfa nyembambaaa; na kubamiza watu kwenye ukuta; na kukanyaga vichwa vya wenzake, almuradi afike huko majuu.
Hajali anamuumiza nani.
Watu aina hii, siku za nyuma, wakitoa ndugu au mzazi, au hata mwana, kwenye kikola; uradi wake utimie.
Unawezakuta ana Sijida kubwa kama tochi ya wachimbaji madini. Isipokuwa tochi yake haitoi mwanga, yatoa giza. Hasbia’Allah! Hatari haswa.
Ukiona hajaachana na mkewe hata baada ya miaka 20, ufahamu kuwa ‘Lao Moja’.
Mume na Mke wana uradi same to same.
▪︎ Sauti ya bomba– hii ni mbiu ya mgambo; au redio bomba.
Wanaotaka kuchafulia hadhi na staha na heshima na utu wa wenzao, hutumia redio bomba.
Watu aina hii wanakuwa na hulka ya kupata starehe yao wanapochafulia wenzao.
Na sheitani amewapa nguvu ya ghilba, akisema uongo wazi wazi, ndimi yake kama kaipaka dawa ya kansole.
Ogopa mtu wa aina hii.
Waswahili tunao usemi “Bora mchawi kuliko Fata’ani”.
Ukilogwa, utaenda kwa Fundi kutibiwa upone.
Au utafanyiwa maombi na sala na unapona.
Fitina haina dawa isipokuwa muathirika wa fitina afunge kibwebwe; aingie ulingoni; aanze vita kupigana na uovu.
Vita aina hii inahitaji umakini, kama vita ya msituni.
Afu unaongeza manyanga.
Fata’ani akitumia ramani ya vita ya phalanx, hii akitumia Phillip wa Macedonia; wewe inabidi utumie Chakravyuh ya Arjun wa Mahabbarata.
Kwa sababu simpo tu- yeye anakuwa na watu wanaomsaidia na kumpa nyenzo, na nguvu.
Wewe unakuwa na Mwenyenzi Mungu.
Inabidi ufanye tawakkal, uingie kwenye medani ya vita kwa mguu wa ‘Namtanguliza Mwenyenzi Mungu’, vinginevyo, huyo afriti hutomweza.
Tena, unapoingia kwenye uwanja wa mapambano, ukubali ‘Ama yeye, Ama mimi’.
Hapo ndo utamweza.
Ndo maana Waswahili huwa tunatanguliza rai kuwa Choko Choko Mchokoe Pweza, Mtoto wa Tanga, Hutomweza.
Together We Can Make it Happen
Leave a Reply