KANSA YA TITI

KANSA YA TITI

IFIKAPO Oktoba kila mwaka, wanaharakati wa Haki Afya huwa tunaadhimisha mwezi wa kusambaza elimu jamii juu ya saratani ya titi.
Aidha, tunakumbuka wapendwa wetu; wanawake wenzetu; mabinti zetu; waliotangulia mbele ya haki, kutokana na saratani ya titi.
Mwezi Oktoba inakuwa kama ni kilele cha mchakato ulimwenguni, wa kueneza elimu jamii, na uelewa juu ya saratani ya titi.
Ukweli usiopingika, miezi yote, tunatakiwa tusambaze ujumbe kwa jamii jinsi saratani ya titi inavyoweza kupona, iwapo wanawake tutachukua tahadhari mapema, ya kupima; na kupata tiba iwapo mmoja wetu amekutwa na saratani ya titi.

Shirika la Afya Duniani WHO limeweka bayana kuwa saratani ya titi, ndiyo inayoongoza kwenye vifo vya wanawake, kutokana na saratani.
Asasi ya CDC ya Marekani imekadiria kuwa kwenye kila wanawake 8, mmoja anaweza kupata saratani ya titi, huko Marekani; ndiyo maana wameweka msisitizo juu ya kupima kila miaka 2-3 ili kufahamu hali ya afya zetu.
Kipimo kinaitwa mammography, na hapa JMT vipo vituo vya kupima wanawake, kuweza kubaini kama wanayo saratani ya titi.

Miaka ya nyuma, sisi Wabongo tukichukulia saratani ya titi kuwa ni ugonjwa unaotokana na kulogwa.
Hii haimaanishi kuwa dawa asili za kutibu saratani hazipo, kwa sababu imegundulika zipo dawa za asili na jadi zinazotibu saratani aina kadha, ikiwemo, tezi dume.
Lakini, walaakin inatokea pale ambapo wagonjwa wa saratani ya titi, hawapati dawa husika za asili, na kupelekea saratani kusambaa kwenye sehemu nyingine za mwili.

Kwa sasa, takriban wanawake wengi huenda kwenye vituo vya afya vya kisasa, kupata dawa na mionzi, ili kuponesha saratani.
Wanawake wengi wamepona, na wameambiwa na madaktari bingwa wa saratani, kuwa sasa, ‘wamepona kabisa saratani’.
Muhimu, ni kupima, na kupata tiba haraka, kabla saratani haijasambaa kwenye mwili.

Wanawake wanaougua saratani ya titi wanapitia changamoto nyingi, zikiwemo:

■ Khofu, wanapopima na kuambiwa wanaugua saratani ya titi.

■ Upatikanaji wa tiba- wengine inabidi wasafiri kutoka vijijini, kuja kwenye majiji, hasa Dar es Salaam, ili kupata matibabu.
Hii inaleta gharama, na inabidi wawepo ndugu wa kuwasaidia.

■ Kukatwa titi/matiti, kunamfanya mwanamke kutojiamini, na kujihisi amepoteza ujanajike wake.
Hapa, panahitajika ushauri nasaha kwake; kwa wanafamilia; na kwa mume, iwapo ameolewa.
Tumeshuhudia wanaume wengi wakitelekeza wake zao wanapokatwa matiti kama sehemu ya tiba ya saratani ya titi.
Hii inaumiza hisia za mwanamke.

■ Ndugu kuchoka kumhudumia mgonjwa wa saratani ya titi, au saratani yoyote ile.
Hapa, viongozi wa dini wanao mchango muhimu wa kutoa nasaha kwa waume, na wanandugu wa mgonjwa wa saratani, kuwa wasimtelekeze.

■ Wanawake walioajiriwa, mara nyingine, hupewa notisi waache kazi, kwa sababu inabidi mgonjwa aende hospital kupata tiba mara nyingi, na pia mgonjwa huchoka na inabidi apumzike.

■ Biashara nazo zinadorora kutokana na ugonjwa.

Nini Kifanyike?

● Asasi ya Tanzania Breast Cancer Foundation ifungue matawi kila mkoa, ili kutoa huduma ya ushauri nasaha kwa mgonjwa; mume/mpenzi; wanafamilia.

● Wanawake tufundishwe jinsi ya kujicheki matiti, kuangalia kama pana uvimbe kwenye matiti au karibu na kwapa.

● Ugonjwa wa saratani usiwe mwiko kuongelewa.
Tuwe wawazi, hadi kwenye mitaala ya shule, mabinti na vijana wafundishwe kuhusu saratani.

● Tujitahidi kuwa na huruma iwapo mwenzetu anaugua saratani ya titi, badala ya kunyoosheana kidole.

● Siyo uvimbe wote kwenye matiti ni saratani, lakini ni bora kuchukua tahadhari na kupima kwa wataalam.

● Saratani SIYO mwisho wa maisha, wala SIYO sertifiket ya kifo.
Ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine, hivyo, anaeugua saratani, asife moyo wala asikate tamaa.
Wanaopona ni wengi, kuliko wanaopata umauti.

● Saratani ya titi siyo ugonjwa wa kuambukiza, hivyo, tusinyanyapae wenzetu.

● Madaktari bingwa wa aesthetics surgery wanaweza kutengeneza matiti upya.

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *