TUJIULIZE

TUJIULIZE

Je sisi wanawake ni malaika? Au tunachangia kwa kiasi fulani, kwenye mmonyoko wa mahusiano ya kindoa/kimapenzi?

TULIPOANZA harakati za kumkomboa mwanamke kutoka kwenye:

  • Ndoa yenye ukatili
  • Mahusiano ya kimapenzi yenye kuumiza nafsi, na hisia
  • Ufinyu wa fikra, kwa kuamini kuwa ‘wanawake tumeumbiwa mateso’ hivyo, tukubaliane na hali tunamojikuta
  • Kutofikiria nje ya kishubaka, kwa kuamini kuwa ‘bila ya kuwa na mume, mwanamke anakuwa hana hadhi wala staha kwenye jamii
  • Kujikwamua kutoka mduru wa umasikini
  • Kujitengenezea miradi ya kiuchumi, nje ya miradi ya pamoja, ya wanandoa, kwa kukhofu kuwa iwapo ndoa itavunjika; au mume akitangulia mbele ya haki; tutakosa hisa zetu kwenye mali ya wanandoa; hivyo, kupelekea baadhi ya wanawake kuanzisha miradi yao binafsi, ya kupata vipato, ambavyo ni vya kwao binafsi.
    Mara nyingine, kuficha waume kuwa wameanzisha kamradi pembeni, ili uwe ni tegemeo lake, siku ya siku, pakitokea utengano; au umauti
    Nk

Sisi wanaharakati, mwanzoni tulijikita kumkomboa mwanamke; na kulinda watoto.
Mwanaume, tukachukulia ‘atajikimu mwenyewe’.

Hii ilikuwa miaka 25-28 nyuma, na harakati za utetezi tulizikita kwenye mustakabala wa maslahi ya wanawake.

Kwenye hii miaka 12-20 nyuma, wanaharakati tumegundua kuwa ili tuweze kupata mafanikio, lazima wanaume tuwaingize kwenye harakati kama wadau, wenye haki sawa kama wanawake.
Palitokea ubishani baina ya wanaharakati.
Wapo waliokataa mbinu hii, na kusema “wanaume weshapewa fursa za kutosha, sasa zamu ya wanawake kupewa fursa, ili tufikie ile 50-50 tunayoilenga kati ya wanawake na wanaume, kwenye nyanja zote.

Tupo sisi, ambao tuliosema kuwa ‘Kampeni zote, iwe kutokomeza ugomvi na ukatili wa kijinsia; ukeketaji; kupunguza na hatimaye kuondoa umasikini; na kujenga jamii zenye kuzingatia heshima; staha; hadhi; utu; wa wanajamii wote, lazima wanaume tuwaingize kama wadau kwenye harakati.
Aidha, tuwasikize, ili tuweze kupata maoni yao, na pia tuweze kutambua changamoto zipo wapi, kuweza kupata ufumbuzi.
Wengine, mimi mmojawapo, tukaitwa Kuwadi wa Mfumo Dume.
Wala haikutukera. Kila vita lazima pawepo na makombora ya maneno!

Hivi sasa, mataifa kadha ya Afrika, yameanzisha programu zinazohusisha wanaume kwenye harakati.
Mfano:

■ Fathers against Female Genital Mutilation FGM.
Ni imeleta mafanikio kwenye mchakato wa kupunguza, na hatimaye, kutokomeza ukeketaji.

■ Men against wife/Intimate Partner Violence IPV.
Bila ya kuwa na wanaume kwenye kampeni za kutokomeza ukatili wa kijinsia majumbani, hatutofanikiwa.
Hivyo, wanaume sasa wameingizwa kwenye kampeni hizo.
Matokeo yake, ikajagundulika kuwa wanawake nao huchangia kwenye ukatili wa kijinsia, kwa kudhalilisha wanaume kwa kauli na matusi.

■ Men against rape.
Program hii imefanikisha kuongeza uelewa juu ya ubakaji wa wanawake; unajisi wa watoto; na ubakaji wa wanaume unaofanywa na wanaume wenzao.
Kumbe baadhi ya wanaume ni waathirika!

■ Men against breast cancer.
Hii imesaidia wanaume ambao wake zao/wapenzi wao wenye saratani ya matiti, wapate ushauri nasaha, na waweze kusaidiana kama familia.

■ Men against cervical cancer- wanaume wanakubali kupigwa chanjo ya kuzuia maambukizi ya HPV, inayosababisha cervical cancer kwa wanawake.
Orodha ni ndefu.
Mataifa kama Uganda; Kenya; Afrika Kusini; yameanza mchakato huu, wa kuwaingiza wanaume kama wadau muhimu, kwenye vita dhidi ya uonevu, au jinsi ya kukabiliana na ugonjwa kwenye familia.

Hapa kwetu JMT, tunaofanya kampeni wanaume waingizwe kama wadau muhimu kwenye kampeni za Haki Jamii, tunaitwa Kuwadi wa mfumo Dume.

 

Tujadili

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *