Mzuri na Mnyama Pori – Beauty and the Beast
NILIPOKUA mtoto, nikipewa orodha ya vitabu vya kusoma, ili niweze kujifunza kusoma, wakati huo, pia najifunza lugha ya Kingereza na Kiarabu.
Nilianza kufundishwa ABJAD ya Kilatini na ABJAD ya Kiarabu kuanzia umri wa miaka 2.
Ilikua kwa sababu niweze kusoma Kiswahili na Kingereza, na pia niweze kusoma Qura’an Majeed kwa lugha ya Kiarabu.
Nawashukuru wazazi wangu na walimu wangu kwa hili.
Tukirudi kwenye vitabu nilivyoanza kusoma, palikua na orodha ya vitabu ambavyo nilipangiwa na walimu nisome ili nijifunze lugha ya Kingereza.
Vitabu hivi nilivisoma usiku na mchana, baadhi vikiwemo:
- Doa Jeupe- Snow White. Hapa nilijengewa hisia kuwa weupe kwa binti na mwanamke ndiyo kigezo cha uzuri.
- Cinderella- Kisonoko. Hapa nilijengewa hoja kuwa daima, ndugu wa kambo ni adui.
- Rapunzel- Manywele. Hiki kilijenga imani kuwa nywele ndefu, laini, zinazoanguka kufika kiunoni, ndiyo ishara ya utanashati na uzuri.
- Beauty and the Beast- Mzuri na Mnyama Pori. Tamthiliya hii ni ya kujenga uvumilivu kwa binti.
Mume anapompiga, anapombagaza, anapoumiza hisia za mwanamke, upendo na stahmala, ni muhimu.
Kwa sababu tamthiliya ya Mzuri na Mnyama Pori inaonesha jinsi Mzuri alivyostahmili kudundwa, eti kwa sababu yule mume, Mnyama Pori, alikua amelogwa na mwanga ili ageuke kuwa na tabia ya kupiga na uonevu.
‘Siyo kosa la Mnyama Pori, kosa la mchawi (mwanamke) aliemloga’.
Nilianza kusoma vitabu hivi kwenye umri wa miaka 4.
Nikawa na njozi za mchana kuwa nikikua na kuolewa na Mnyama Pori, nitampa upendo mwingi sana, hata akinibamiza kwenye ukuta, nitampenda na kumstahmilia, kwa sababu Mzuri ndivyo alivyofanya.
Nilipofika umri wa miaka 12, nikapewa kitabu na Mwalimu wangu ambacho kilibadili mtazamo wangu juu ya njozi ya kuwa na Mnyama Pori, hata awe katili iweje, mapenzi yakubali huo ukatili.
Kitabu nilichopewa kusoma kwenye umri wa miaka 12 ni The Female Eunuch alichoandika Germaine Greer.
Nilipoanza kukisoma, nadharia nyingi kwenye kitabu sikuzielewa. Zilikuwa ngeni kwangu, hasa kwenye umri wa miaka 12, na, sijawahi kuzifikiria nadharia aina hiyo. Kuwa binti anafundwa kukubali kupigwa na huyo Mnyama Pori, ndani ya familia yake, na kuwa hapo ndipo mabinti wanapijengewa hisia za kutojiamini.
Kitabu The Female Eunuch nilikisoma, na kurudia kukisoma mara 6.
Baadaye nikapewa vitabu vingine nisome ambavyo vilinipa taswira ya wanawake ambao wanaumia hisia, miili, uwezo wa kifedha, kukosa hadhi kwenye jamii, na mara nyingine kutengwa na jamii, lakini hao wanawake hujikaza na kuanza maisha upya, na wanajiinua pole pole, mpaka wanakaa sawa kimaisha, mara nyingine, wakiwa na watoto.
Nilipokuwa nasoma Ungereza kwenye umri mdogo, Mwalimu wangu Dr Anne Phillips alinipatia sehemu ya kujitolea- Fawcett Library, ambayo ni maktaba mkubwa kuliko zote ulimwenguni, yenye vitabu juu ya wanawake; na vingi vilivyoandikwa na wanawake. Nikienda kwa wiki mara 2 kujitolea kupanga vitabu wanavyorudisha wanachama wa maktaba.
Palinifungua macho. Kuwa mwanamke anaweza kuanza maisha upya, hata kama amepata misukosuko ya kubakwa au kufanyiwa kashfa na vitendo vya aibu.
Mwalimu mwingine, Ms Dana Sperakis, alinipatia sehemu, Chiswick Crisis Centre niweze kujitolea kama volunteer kusaidia wanaosaidia wanawake wenye kupitia mateso kutoka kwa wapenzi au wanandoa, Intimate Partner Violence IPV.
Nilifundishwa jinsi ya kuchukua maelezo, na jinsi ya kumfariji mhanga wa matukio hayo.
Hii no elimu muhimu. Nawashukuru walimu wangu. Sina cha kuwalipa, isipokua niliwaahidi nikirudi JMT, nitaandika makala na vitabu kuondoa ugaga na utandabui unaowekwa kwenye fikra za mabinti kuwa Mzuri lazima avumilie mateso kutoka kwa Mnyama Pori.
Siyo kosa la Mnyama Pori, alilogwa na mchawi ndiyo kugeuka na tabia za mnyama.
Tukirudi kwa Mzuri na Mnyama Pori, hizo ni tamthiliya ambazo kwenye miaka ya mwanzoni 1990s baada ya kumaliza kusoma, TAMWA tulijaribu kuzigeuza na kumfanya Mzuri kuwa mkakamavu kwa kuandika makala na tamthiliya zinazoonesha Mzuri anavyokataa kudundwa na kutusiwa.
Binafsi niliandika vitabu 4 kwenye msalsal/series Visa vya Kurwa na Doto kuanzia 1993-1995.
Mwana TAMWA Pili Mtambalike akaabdika Wimbo wa Sandina.
Mwana TAMWA Chemi che Mponda aliandika Miwa. Nilikuwa mhariri wa vitabu na gazeti TAMWA, na wana TAMWA waliandika:
- Vitabu
- Makala maalum- haya waliandika waandishi nguli Dada Ichikaeli Maro; Wii Khadija Riyami; Dada Pude Temba; Dada Rose Kalemera; na wengineo.
Watayarishaji wa vipindi vya redio akina Teacher Rose Haji Mwalimu; Mama Eda Sanga; Da Marie Shaba; Dada Valerie Msoka na wengineo, walitengeneza vipindi kuvunja ule mfumo wa Mzuri kustahmili mateso kutoka kwa Mnyama Pori.
Watayarishaji wa vipindi vya luninga akina Dada Fawziyat Aboud; Mama Anna Idrissou; Dada Rebecca Mngodo; Dada Sarah Luhindi; wakatengeneza vipindi vyenye kumwonesh Mzuri akikataa vipigo na mateso ya hisia. - Tulitoa majarida yetu wenyewe.
- Tukatoa vipindi vyetu wenyewe
- Tukaandika na kuchapisha vitabu wenyewe
Hapo hapo, tukawashirikisha Wahariri wa vyombo vya habari, na wanahabari kwenye Kampeni ya kuweka taswira ya mwanamke kwenye mintarafu ya heshima na staha na utu.
Sasa, tunaona wimbi la wasichana wanaovalishwa vichupi tu na kuchezeshwa JEJE kwenye video za nyimbo.
Tunajiuliza Zile jitihada zetu za kuvunja mfumo wa Mzuri kuvumilia mateso ya Mnyama Pori zimekwenda kwa maji?
Tutafakari,
Leila Sheikh
Tanga,
Novemba 24, 2021
Leave a Reply