SHUKRANI
NYOYO zenye shibe na nafsi zenye shukrani, zinakuwa zimekidhi matakwa ya Mwenyenzi Mungu, kuwa majaribu ni sehemu ya maisha yetu, na sisi, hatutakiwi kukata tamaa; wala kuvunjika moyo; kwa sababu, hata Mitume kwenye Misahafu Takatifu, walipewa majaribu, na ilibidi waombe kwa Mwenyenzi Mungu, awavushe kutoka hayo majaribu.
Tatizo letu sisi binadamu, tumeumbwa na mapungufu, ambayo huwa mara nyingine, yanapindukia, hadi kusimanga wenzetu ambao hawanacho; kwa kuamini kuwa sisi, tulichonacho, ni kutokana na himaya yetu.
Tunasahau kuwa ufalme wote ni wa Mwenyenzi Mungu.
Vya mbingu na ardhi vyote ni vya Mwenyenzi Mungu.
Na hakuna binadamu ambaye hatapitia kipindi, au vipindi, vya majaribu.
Hivyo, iwapo mwenzetu anapitia kipindi cha majaribu, sisi, tunatakiwa kumsaidia; hata kwa kauli ya kumpa hima na tumaini.
Wengi wetu hunyoosha kidole na kucheka “Kiko wapi? Yule aliepanda inter cooler VX sasa apanda bajaji”.
Hapa, hatumsimangi yule mwenye matatizo, bali tunakosoa maamuzi ya Mwenyenzi Mungu.
Waswahili tunausemi “Mpaji Mungu”, na daima, tunatakiwa tuwe na unyenyekevu kwa Mpaji, ili atuongezee neema; na atuvushe kutoka kwenye majanga.
Tunawaangalia Waheshimiwa wetu Bungeni, na baadhi yao, tunawaona wamejiweka mbali na majimbo yao; ambao ni sisi, wenye nchi yetu.
Wengi wao, wakishapata posho zao; na mishahara: marupurupu; na lebo sijui cheo, cha kuitwa “Mhe”, wanasahau kuwa wasingepata yote hayo, bila ya sisi, wenye nchi yetu kuridhia.
Wachache sana hukumbuka majimbo yao, jambo la kusikitisha.
Tunawaangalia.
“Cheo ni Dhamana” nadhani hii ilikuwa Kauli Mbiu ya CCM wakati sisi ni watoto.
Waheshimiwa wangerudi huko na kuitafakari Kauli Mbiu hii, ili kuondoa mapepo mabaya ya cheo kupanda kichwani.
Turudi kwenye Misahafu Takatifu, pale Mwenyenzi Mungu anapotuelekeza binadamu kuwa Ufalme anatoa Yeye Mwenyenzi Mungu, na anaweza akauchukua muda wowote, anapoamua hivyo, sisi, tujinasibishe miongoni mwa wanaomcha Mwenyenzi Mungu, na wanaoogopa hasira ya Mwenyenzi Mungu.
Sisi, wananchi tupo.
Tujadili,
Together We Can Make it Happen
Leave a Reply