Celebrating the Two great Swahili Women- Siti bint Saad and Bibi Titi Mohamed
▪︎ “Nilikwenda Zanzibar mwaka 1942, kwa meli. Alinichukua mume wangu wa pili, Bwana Mahmoud. Sijawahi kuona ukarimu aina hiyo.
Nilikaribishwa nyumbani kwa Bi Jokha Steiner, alikuwa mke wa Seyyid Sood, lakini alitoka huku Bara, Tanganyika.
Alialika mabibiye chai ya usiku.
Ma sha Allah, ukiingia, unapokewa baibui; unapewa kanga za kujitanda. Unafushwa udi, unapakwa uttur kwenye mikono.
Chini pametandikwa matiffe mazuri, ya kila rangi.
Taqia na mito ya kuegemea.
Ukiingia unakaribishwa kwa ‘Salaam’.
Kwanza tukanawidhwa kwa mideli na birika za maji yenye asumini. Tukapewa sharbat ya maziwa yenye lozi, na vipopoo vidogo.
Wakapitisha tambuu na sigreti, huku tumeegemea taqia.
Kila ajae, anatoa Salaam.
Baadaye, wakaleta kila aina ya chakula na sharbati za matunda. Huku, mpiga kinanda anapiga bashraf.
Baada ya kumaliza kula, ndiyo akaingia Al Anisa, Siti bint Saad, na ushungi wake.
Alikuwa hapendi kula kabla hajaimba. Akila baada ya kuimba.
Akinywa tangawizi yenye asali.
Nikatambulishwa kwa Siti bint Saad.
Mpiga kinanda akaanza kupiga wimbo wa Siti bint Saad, unaitwa ‘Siku hizi’.
▪︎ Siti bint Saad aliimba nyimbo tatu tu, lakini kwa ile sukaina (tranquillity) tuliopata, utadhani aliimba nyimbo 30.
Siti bint Saad hakula tambuu, wala hakuvuta sigara.
Alikuwa mpole, si msemaji sana.
Akitabasamu.
Nikakaribishwa niimbe, Looh! Mie Titi, niimbe mbele ya Melki wa Taarab, Siti bint Saad?
Nikajikusanya, nikamwelekeza mpiga kinanda kuwa nitaimba wimbo wa Kiarabu, nikaimba ‘An Bahebak’.
Mabibiye walikuwa wanatuza rupia”.
▪︎ Siti bint Saad akaingia kati kati, naye akaimba pamoja nami, tukawa tunatunga hapo hapo, tenzi za wimbo kwa Kiswahili”
Bibi Titi Mohamed
1998
Upanga,
Dar es Salaam
The Bibi Titi notes, Leila Sheikh
Leave a Reply