Ukatili wa kijinsia dhidi ya walemavu

Ukatili wa kijinsia dhidi ya walemavu

DESEMBA 3 tunaadhimisha Siku ya Watu wenye Uwezo Tofauti, ambao wengi wetu huwa tunatumia msamiati wa kuwaita Walemavu.

Ni Siku ambayo tunatakiwa kufanya yafuatayo:

■ kutambua uwepo wa watu wenye uwezo tofauti/walemavu, na jamii inayowazunguka.

■ kufanya tathmini ya Mipango ya Taifa ya mwaka uliopita, na kuangalia tumepiga hatua ipi kwenye kuendeleza maisha ya walemavu; mapungufu yaliyopo kwenye Mipango na Mikakati yetu kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu; na nini kifanyike kuongeza juhudi, kwenye kuwapatia walemavu huduma stahiki, ili waweze kuishi maisha yenye tija na maendeleo yao.

■ Kutoa Taarifa ya Mipango ya mwaka unaokuja juu ya mustakabala wa watu wenye ulemavu.

■ kuzungumzia umuhimu wa kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi, dhidi ya watu wenye ulemavu.

■ kukumbushana kuhusu Haki za Msingi za watu wenye ulemavu, ambazo ni haki kama za wananchi wote; zilizoainishwa kwenye Katiba ya JMT, kwenye Fungu la Haki za Msingi-

▪︎ Haki ya kuishi bila bughudha; ubaguzi; unyanyapaa

▪︎ Haki ya kupata huduma ya afya

▪︎ Haki ya ajira na ya kupata ujira, kwa kazi au biashara wanazofanya

▪︎ Haki ya kuoa au kuolewa

▪︎ Haki ya kuwa na watoto, iwe wa kutoka kwenye mwili wake; au watoto wa kulea

▪︎ Haki ya kupata pango la nyumba

▪︎ Haki ya kusafiri

▪︎ Haki ya kufurahia maisha

▪︎ Haki ya kujipodoa

▪︎ Haki ya kupata elimu

▪︎ Haki ya kupewa heshima na staha na faragha ya maisha yao

▪︎ Haki ya ulinzi wa maisha yao; mali zao; uhai wao; usalama wao dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Bado Taifa hatujaweka Mikakati na Mpango maalum, wa kuwapa ulinzi wenye ulemavu, dhidi ya ukatili wa kijinsia.

■ Tukiangalia kwenye matokeo ya tafiti tulizofanya, wenye ulemavu, hususan wanawake na watoto; wapo kwenye mazingira hatarishi ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia, tukilinganusha na wananchi ambao hawana ulemavu.
Hii inatokana na walemavu kuwa na uwezo tofauti na wanajamii wengine.
Mfano, mwanamke mwenye ulemavu wa viungo, inamuwia vigumu kukimbia; au kuminyana; na mbakaji, kwa jinsi maumbile yake yanakuwa na changamoto.

Walemavu wa kusikia na kusema, wakienda kutoa ripoti polisi, wanashindwa kujieleza, kwa sababu hatujaweka Dawati makhsus kwa wenye ulemavu; na hatujaweka wakalimani wa lugha ya ishara kwenye vituo vya polisi.
Muathirika akienda kutoa ripoti kwa lugha ya ishara, inabidi aoneshe kitendo kilichomtokea, kwa njia ya ishara, ambayo hufanya watu wamcheke, kwa sababu anaonesha tendo la ngono la ubakaji.
Hii inaleta simazi na majonzi kwa mlemavu aliebakwa, kuwa ametendewa uovu huo, na anachekwa akijitahidi kuelezea askari polisi, juu ya madhara aliopata.

■ Mlemavu wa kusikia na kusema anashindwa kupiga kelele kuomba msaada, akifanyiwa shambulio la aibu.
Anabaki kuguna, machozi yanamtiririka.

■ Walemavu wa usonji huwa hatuwapi elimu jamii juu ya ukatili wa kijinsia, kama ubakaji; Unajisi wa watoto.
Hili ni pungufu kubwa, ambalo inabidi tulipangie mikakati, kuwapa watoto wenye usonji, waelewe wanaposhikwa sehemu za siri, wasikubali.
Watoe taarifa kwa wazazi/walezi wao.
Watoto wenye ulemavu wapo kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kunajisiwa; kubaguliwa; kunyanyaswa; kuliko watoto ambao hawana ulemavu.

■ Hatujaweka mikakati kusaidia wenye ugonjwa wa akili, na jinsi ya kuwalinda, dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mgonjwa wa akili anakuwa kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia, kuliko watu wasio na ugonjwa wa akili.

■ Kupiga mawe watu wenye ulemavu hutokea.
Inasikitisha mno.
Hata paka hapigwi, seuze binadamu wenzetu.

■ Wanawake wenye ulemavu wa viungo au kusikia au kuona, mara nyingi hupata manyanyaso na masimango, ndani ya ndoa au ndani ya mahusiano ya kimapenzi.

■ Wenye ulemavu wa viungo wanahitaji vyoo rafiki; vyenye stara; kurahisisha kuweza kujisaidia.
Tuweke Mpango kuwa kila Ofisi ya umma; AZAKI; sehemu za ibada; sehemu za biashara; shuleni; kwenye vyuo vya elimu ya juu, pawepo na vyoo ambavyo ni rafiki kwa walemavu.

■ Wenye ulemavu wa kuona, wapatiwe nyenzo za kusoma kwa braille; au kupitia kanda za audio.
Na waruhusiwe kufanya mitihani kwa braille; au kwa kutumia kauli.

■ Wazazi wasiwapige; wasiwadulubu; wasiwanyanyapae; watoto wenye ulemavu.

■ Walemavu wapatiwe stadi za maisha, kuhusu wafanyeje, wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia.

■ Madaktari na wahudumu wa hospital wapewe mafunzo ya ushauri nasaha/empathy kwa watu wenye ulemavu.

■ Viongozi wa dini wakemee ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wenye ulemavu.
Si siri, mwanamke mwenye ulemavu anaweza kuchangiwa na wanaume 5, wakampiga mande ya ubakaji 😢.
Na watoto wenye ulemavu wapo kwenye hatari zaidi ya kunajisiwa.

Zipo AZAKI za watu wenye ulemavu; na Shirikisho la asasi za Watu wenye Ulemavu.
Hizi, zisaidiwe Kuweka Mipango kusaidia walemavu kwenye haki na ulinzi.
Mipango ifike hadi ngazi ya jamii.

Kila mmoja wetu ni Mlemavu Mtarajiwa

Nukuu ya Madam Sally Qazi.

Tujitahidi kulinda watu wenye ulemavu dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Together, we can make it happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *