Stress
TUNAPOZONGWA na mawazo hadi kuleta hali ambayo mitaani wanaita vyuma vimekaza au umepata mkazo ni jambo na hisia tunaichukulia kama ‘kawaida’, kwenye maisha yetu.
Takriban mara chache sana, huwa tunaanisha uwepo wa hiyo hali kwenye maisha yetu, hadi kuathiri afya zetu za mwili, na, za hisia.
Stress ni ‘rafiki’ ambaye hatumhitaji, wala hatumtaki, kwenye maisha yetu, lakini, tunae, anaishi na sisi, na mara nyingi, tukimwachia, anachukua utawala wa:
- mawazo
- hisia
- maamuzi
- afya
- utendaji wetu wa kazi
- mahusiano yetu na wanafamilia
- mahusiano yetu na wafanyakazi wenzetu, na wanajamii wenzetu
- jinsi tunavyopangilia maisha yetu
- matumizi ya pesa
- muonekano wetu – tunavyojijali; tunavyo vaa nguo
Kwa ufupi, stress hutawala maisha yetu!
Nini huleta stress/mkazo?
- kuongezeka kwa majukumu
- kuwa na mgonjwa ndani ya familia
- kazini kufokewa mara kwa mara na Wakuu/Mkuu
- kuchukua majukumu mengi, hadi yale yaliyo nje ya uwezo wetu
- migogoro ndani ya ndoa
- madeni
- kukosa ajira
- kuwa na mtoto mwenye mahitaji maalum
- kukosa uwezo wa kujikimu
- kufanyiwa inda ya ngono lazimishi kwenye sehemu ya ajira
- kutoweza kukimu maisha
Orodha ni ndefu, na dondoo kwenye orodha, zote zinazo umuhimu wake.
Stress/Mkazo, unaweza kuleta madhara ya:
- kupata hisia za wasi wasi
- kichwa kuuma
- mapigo ya moyo kuongezeka
- kukosa usingizi
- kusononeka
- hasira za kila mara, hasa kuwatolea maneno au matendo ya ukali, watu wa karibu
- kukaripia watoto, na mara nyingine, kuwapiga
- kutafuta ugomvi na mpenzi au mwanandoa au ndugu au rafiki
- kula sana hadi kunenepa au kuacha kula kabisa
- kunywa pombe bila kipimo
- kulia mara kwa mara
- kununua vitu usivyohitaji, na kujiongezea mzigo wa madeni
- kutooga au kutojitunza umaridadi
- kutotamani kuonana na ndugu au rafiki
- kujigungia ndani peke yako
NK.
Wataalam wameweza kuainisha vifumua stress/mkazo, au ‘triggers’ kwa lugha ya Kingereza.
Hivi vifumua stress tunaweza kuangalia, na kuvifahamu, kwenye maisha yetu, na kuweza kukabili hiyo hali, na kuirekebisha.
Muhimu
- kutambua nini kinacholeta stress/mkazo kwenye maisha yako, na kujaribu kupata ufumbuzi
- kuongea na ndugu wa karibu au rafiki, ili upate ushauri
- kujikinga dhidi ya madhila ya maisha, mfano, migogoro ya kwenye ndoa/mahusiano ya mapenzi
- kutoa ripoti iwapo unafanyiwa tendo la ngono lazimishi kwenye sehemu ya ajira, au kwingineko
- kusali na kufanya ibada
- kutengeneza na kuandika kwenye kitabu/notebook orodha ya changamoto unazopitia.
Baada ya hapo, kutengeneza orodha na kuandika mambo yaliyo mazuri kwenye maisha yako.
Utakuta mambo yaliyo mazuri kwenye maisha yako ni mengi zaidi, na yenye kuleta tumaini, kuliko changamoto ulizonazo.
Binadamu tumejenga kawaida ya kuangalia yaliyo mazito kwenye maisha, na hatuangalii yaliyo mazuri na yenye kufurahisha.
Tunasahau kuwa hata kusikiza muzeka, kunaleta furaha.
Kuangalia maua yalivyochanua huleta tabasamu.
Kula muhogo wa kuchemsha na kachumbari ni yummy.
Kusali na ibada huleta faraja.
Kuwa miongoni mwa watu wanaotujali ni majaaliwa.
Kuwa na shukrani ni njia kubwa ya kujikwamua kutoka kwenye stress/mkazo.
Tujitahidi
- kutonunua vitu/bidhaa ambavyo hatuna uwezo navyo, na mara nyingine, wala hatuvihitaji
- kuwa na uelewa juu ya stress triggers, na kuchukua hatua tusiingie kwenye mzunguko utakaotufanya tudidimie kwenye ugonjwa
- tuweke orodha na mahesabu ya fedha tunazopata kwenye ajira/biashara, na mahitaji yetu ya matumizi.Baada ya hapo, tujitahidi tuishi ndani ya misingi ya uwezo wetu. Siyo lazima uwe na gari la kifahari, linalohitaji mafuta na matunzo ya gharama.Wengi wetu tunapanda dala dala, na bado hadhi zetu zipo pale pale
- kununua mapazia ya mtumba siyo jambo la aibu
JITAMBUE
Unapoona unaanza kuingia kwenye mduru/cycle inayoleta stress/mkazo, haraka, jihusishe na kitu kinachokufariji.
Siyo pombe wala kutafuta mabwana wa kukuliwaza, bali ingia ndani ya nafsi yako mwenyewe, ujikwamue.
Sala, ibada kwa ujumla, husaidia sana.
Kumbuka, hauko peke yako.
Binadamu wote hupitia changamoto.
Jinsi ya kukabiliana na changamoto hutofautiana, lakini tusikubali kutekwa nyara na stress/mkazo.
Tujikinge.
Leila Sheikh
Desemba 16, 2021
Leave a Reply