Watoto kwenye Omba Omba

Watoto kwenye Omba Omba

MWAKA jana 2021, tulipata taarifa kuwa wapo watoto kutoka JMT, waliopelekwa Kenya, kufanya kazi ya omba omba.
Aidha, tulipata taarifa kuwa watoto hao ni miongoni mwa wale wanaosafirishwa kwenye biashara haramu ya uuzaji wa binadamu.
Binafsi, nilihojiwa na redio ya VOA kuhusu suala hili, na mwanahabari mwenzangu wa Kenya; na mwanaharakati wa ulinzi wa watoto huko Kenya; walitoa ushuhuda kuwa watoto hao wanaotumikishwa kwenye omba omba, wanadai wanatoka JMT.
Nikafatilia hapa JMT, hususan Tanga, kwa sababu inapakana na Mombasa, Kenya.
Nikaambiwa kuwa ni kweli hao watoto wanaotumiwa kama omba omba ‘waliuzwa’ na kupelekwa Kenya, lakini JMT ni njia/transit ya kupitisha hao watoto.
Takriban wengi wao wanatolewa kutoka Malawi.
Tanga, inakuwa ni transit place ya kuwapitisha, na kuwapeleka Kenya, kufanya omba omba.
Wakiwa Kenya, wakiulizwa, wanasema wanatoka JMT.

Hapa ndani ya JMT, omba omba wanakuwa watoto na wanawake wa Kitanzania, ambao wametolewa vijijini kwao kwa ghilba kuwa watatajirika wakija kuwa omba omba kwenye majiji, kumbe kuwa omba omba hawajifanyii wenyewe, bali yupo mtu au watu, wanaoagiza binadamu wenzao, kufanya ‘ajira ya omba omba’ na pesa inayopatikana, huchukua yule alietuma dalali vijijini, ili kuwaleta hao binadamu wenzetu, wanaofanyishwa kazi ya omba omba.

Omba Omba ni njia mojawapo ya utumiaji watoto kwenye ‘ajira ya watoto’; tena ajira ambayo ni hatari kwa watoto hao.
Siyo tu kuwa omba omba/loitering/soliciting ni kosa kwa sheria zetu, lakini hao watoto wanakuwa kwenye mazingira hatarishi.
Mifano:

▪︎ Wanaweza kunajisiwa, na mara nyingi hunajisiwa, kwa watoto wa kike na wa kiume

▪︎ Wanapigwa na wanaowatumikisha, na pia na watu wanaowaomba pesa

▪︎ Wanakuwa hawana malazi, wanalala barabarani, nje ya maduka au maofisi

▪︎ Wanakuwa hawapati fursa ya kusoma

▪︎ Wanapoumwa, hawapelekwi hospital, na wengi wao, wanaugua taabani, lakini inabidi wafanye omba omba, ili kila jioni, wampe fedha yule ‘aliewanunua, na kuwafuga’ kwenye utumwa mamboleo, wa kufanya kazi ya omba omba

▪︎Wanapojaribu kutotoka, hufatwa na kupigwa, na kurudishwa barabarani, kwenye omba omba.

▪︎ Maisha ya omba omba ni magumu mno.
Tunafikiri wanakuwa omba omba kwa sababu ya uvivu, kumbe hawa ni watumwa mamboleo, wanaotumikishwa kuwa omba omba; kukusanya fedha kwa ajili ya ‘tajiri wao’ aliowalipia nauli na pesa za dalali, ili kuwaleta kwenye majiji.

Maisha ya omba omba hayana fursa ya binti au kijana kuwa na ndoto, za kujikwamua kutoka kwenye umasikini, na kuweza kujiendeleza.
Omba omba anaishi siku hadi siku.
Mara nyingi wanasahau hata ni siku ipi kwenye wiki, au ni mwezi upi kwenye mwaka.
Wao ni kuamka alfajiri kutoka kwenye virago vya maboksi na matambara waliookota kwenye jalala, na kuanza omba omba.
Mara nyingine, hata chakula hawapewi.
Labda itokee mwenye mgahawa kuwaonea huruma, na kuwapa maandazi au mikate.
Wengi wao omba omba wanasahau desturi na mila, kwa kuishi barabarani.
Huu ni moja ya utumwa mamboleo.

Tujadili

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *