Ubadhirifu na Utumiaji Mbaya wa Madaraka

Ubadhirifu na Utumiaji Mbaya wa Madaraka

BADO WABONGO hatujapatiwa elimu jamii juu ya ubadhirifu, na/au utumiaji mbaya wa madaraka.
Jamii zetu hazijapewa uelewa juu ya jinai hii, ya ubadhirifu na/au utumiaji mbaya wa madaraka.
Hata pale panapotokea matendo ya ubadhirifu au/na utumiaji mbaya wa madaraka; wachache miongoni mwetu tunaouelewa kuwa pamefanyika kosa, tena takriban mara nyingi au zote, linakuwa ni kosa la jinai; na hatuna uelewa kuwa tunayo haki; na tunao uwezo; wa kusisitiza huyo alietenda jinai hiyo, achukuliwe hatua za kisheria.
Hii inatokana na Taifa kutokuwekeza kwenye elimu jamii juu ya uelewa wa msingi wa mfumo wa sheria zetu; hadi tukifanya tafiti, tutagundua ni wachache sana miongoni mwetu, wenye kufahamu kuwa tuliowakabidhi dhima ya kusimamia masuala ya mustakabala wetu, wanapofanya kinyume na badala yake, wanatumia vibaya dhima (ambayo wao hupenda kuita madaraka); wakati sisi, watetezi tunaita ‘Kukabidhi Dhima’, wanapofanya maamuzi na matendo kinyume cha Makubaliano baina yao na sisi.
Inasikitisha tunapoona tuliowajabidhi dhima ya kusimamia mustakabala wa Taifa letu adhimu, wakijigeuza au wakigeuzwa Mungu watu.
Inaleta kichefuchefu pale ambapo inatubidi tuwashukuru, eti kwa ‘kumwaga’ fedha kwenye miradi ya maendeleo; wakati hiyo ni fedha yetu sisi, wana JMT, na wao, ni watumishi wetu, tuliowakabidhi dhima hiyo, na tunawalipa.
Taifa linarudi kwenye fikra za utumwa mamboleo; wa ‘kuabudu’ watumishi wetu; wakati sisi, ndiyo wenye nchi yetu.

Alisema Mwanafalsafa Plato, kwenye kitabu chake maarufu ‘The Republic’ kuwa ili tuweze kuishi kwenye Jamhuriya; naweka msisitizo kwenye neno huriya ambalo ni neno zuri na tamu mno- Hur/Huru/Huriya/Jamhuriya; lazima wamiliki hiyo Jamhuri watambulike kuwa wao ndiyo vibosile; na Watumishi, watambulike kama hivyo..Watumishi wa Umma.
Laakin, wanajisahau, tukishawakabidhi nyenzo za utumishi wa umma.
Wanatugeuka.
Mara nyingine, tunaishi kwa khofu dhidi ya hao tuliowaajiri kutufanyia utumishi.
Dah!
Uajiri meneja asimamie shamba lako; uweke na watchman kwa ajili ya ulinzi wako na wa mali yako; afu unaishia kuwasujudia, na kuwaogopa!
Ndiyo maana Mwanafalsafa Thomas More alitayarisha Andiko, akalipa jina Utopia au kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili, Taifa la Ruyya/Ndoto; kwa sababu Taifa aina hiyo lipo kwenye ulimwengu wa ndoto, na siyo kwenye ulimwengu tunamoishi, wa ‘Vuta Nikuvute’. Ulimwengu wa Utopia ni wa kindoto, ndiyo hilo neno Ruyya, ikimaanisha ndoto kwa Kiswahili fasaha cha Nguli wa Malenga, Shaaban bin Robert.
Nahisi neno ‘Maruerue’ limetokana na chimbuko la neno ruyya.

Huko kwenye Taifa la Ruyya, kila mwananchi anatakiwa ashiriki kwenye maamuzi ya mustakabala wa Taifa lake.
Anatakiwa apate fursa zote.
Anatakiwa awe na afya.
Zaidi ya hayo, anatakiwa awe na furaha.
Ndiyo maana pakaitwa Utopia.
Kwenye ulimwengu wa Vuta Nkuvute, tuliowakabidhi dhima ya kuwa watumishi wa umma, wanaanzisha mfumo wa Adhabu na Tuzo au Punishment and Rewards.
Kivipi? Utakuwa unajiuliza.
Kwa kutumia nyenzo tulizomkabidhi, na kutukandamiza tusipomsifia na kumuabudu; na kuwapa bakhshish wale wanaompaka mafuta na kusujudu.
Huu Mfumo umejengeka ulimwenguni pote, hata kwenye mataifa yanayojiita Komavu wa Demokrasia.
Ni ile Utopia ya Thomas More.

Tunaangalia huku twajiuliza “Nani mwenye mali?”
Sisi wenye nchi yetu? Au tuliowaajiri, tukawakabidhi dhima ya kusimamia mustakabala wa Taifa letu adhimu.

Together, we can make it happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *