Grooming- Kurubuni Watoto
PAMETOKEA msamiati mpya kwenye harakati za kulinda watoto dhidi ya kunajisiwa.
Neno Grooming- Kurubuni ndiyo linalotumika kuelezea jinsi mtu mzima anavyotumia ghilba ili kumrubuni mtoto, na kisha kumnajisi kwa mfululizo.
Grooming- Kurubuni huchukua taswira kila aina, ili mtu mzima, aweze kumpata mtoto, wa kike au wa kiume; na kumfanyia vitendo vya unajisi. Mfano:
■ Kufanya urafiki na mtoto, hasa iwapo huyo mtoto anakuwa hapati muda wa kuketi na wazazi/walezi; au mtoto ambaye anakaripiwa sana, na wazazi/walezi, badala ya kupewa salaa na uelewa juu ya maisha mfano masomo.
Mtoto anasononeka.
Hapa ndipo hao Fisi Watu/Predators, watu wazima au vijana wakubwa, hujifanya wanayo huruma juu ya huyo mtoto.
Pole pole, wanamghilibu mtoto hadi wanafikia hatua ya kujenga imani ya mtoto kwa hao Fisi Watu, ndipo Fisi Watu huanza kumnajisi huyo mtoto.
Mtoto anafikiri ‘anapendwa’; anasikiziwa; anajaliwa.
Kwa vile hapati hivyo kutoka kwa wazazi/walezi, mtoto anaamini huyo Fisi Mtu ndiye anaempenda.
Mtoto anakuwa tayari kufanya lolote analoambiwa na Fisi Mtu.
■ Kupatiwa ‘zawadi’ za gharama kubwa, na huyo Fisi Mtu.
Mfano-
> Simu ya smart phone
> Saa ya kuvaa mkononi
> iPad
> Chips Kuku
Nk
Hii hufanywa na Fisi Mtu, ambaye mara nyingi anakuwa mtu aliekaribu na familia, ili kumrubuni mtoto, wa kiume au wa kike.
Wakati huo, wazazi/walezi wanafikiri huyo Fisi Mtu anamjali mtoto wao, kumbe ni njia ya ghilba ili aweze kumnajisi mtoto.
■ Mwalimu wa shule au madrassa au tyusheni, kumkurubia mtoto; kumshika kichwani au kwenye bega; na mara kwa mara, kumsifia mtoto darasani ili kujenga hisia za kujaliwa kutoka kwa mtoto.
Baada ya hapo, kumkaribisha mtoto abaki baada ya masomo, na kumnajisi.
■ Kurubuni watoto kupitia mitandao ya kijamii.
Fisi Mtu hutumia njia hii, na takriban mara zote, wazazi wanakuwa hawana taarifa.
Fisi Mtu anamghilibu mtoto kupitia mitandao ya kijamii, na baada ya kupata trust/imani ya mtoto, humkaribisha wakutane kwenye mgahawa, na baadaye kumnajisi.
■ Kungoja mtoto anaporudi nyumbani kutoka shule au mazoezi, na kumpa ofa ya lifti.
Inageuka mazoea na baada ya hapo, Fisi Mtu anaanza kumnajisi mtoto.
■ kuunda urafiki na wazazi/walezi wa mtoto, hadi anaaminika nyumbani.
Ndipo anapoanza udhalimu wa unajisi wa watoto.
■ Ndugu wa karibu mfano kijana wa shemeji au binamu, kuwekwa chumba kimoja na mtoto, kwa kufikiri kuwa huyu ni wakuaminika, hivyo, alale kitanda kimoja na mtoto.
Hii ndiyo imesambaa sana, na sisi watetezi wa ulinzi wa watoto tukiwaambia wazazi waepuke tabia ya kuwalaza watoto na ‘ndugu’, huwa wanakasirika.
Inabidi mfano mimi, niwakumbushie kuwa “Niliratibu Vituo vya Msaada kwa wahanga wa ukatili wa watoto na wanawake..”
Hata hivyo, huwa hawataki kusikia, mpaka mtoto amedhulumiwa kwa kunajisiwa mara nyingi; ndipo wanaamini.
Wapo watetezi wanaoacha kusema.
Tupo watetezi sisi tunaosema, huku tukifahamu kuwa wazazi/walezi wanaweza kutuchukia, na tumeamua kujitoa mhanga ili watoto wapate ulinzi.
Orodha ya Grooming- Kurubuni ni ndefu.
Inahitaji mijadala kwenye jamii zetu kupitia asasi za dini; vyombo vya habari; na mijadala kwenye mitandao ya kijamii.
Tujitahidi kulinda watoto.
Together, we can make it happen
Leave a Reply