Ni siri? Au batili dhahiri?
Siri, si siri, inapofanywa dhahiri, juu ya uzushi mahiri, bila ya kufikiri wala tafakuri, mwishoe, kugundulika uongo taswiri.
Tenzi ya bint Sheikh
HAPO dakhari zamani, palikuwa na Zumbe huko Tongoni, Tanga, ambaye akivaa kofia ya baragashia, ndiyo alama ya uzumbe.
Zumbe Mwinyi Mkuu alikuwa na kinyozi, ambaye kila alkhamis, huenda qilla (fort/ikulu), kumnyoa Zumbe nywele; kumpunguza ndevu; na kumkata kucha, ili siku ya Ijumaa, Zumbe Mwinyi Mkuu aende Msikitini kusali, kwenye hali nadhifu.
Baada ya Salat’l Jumaa na khutba, Zumbe Mwinyi Mkuu akisimama nje ya Msikiti, na kugawa zakka kwa wasiojiweza.
Zakka ilikuwa mpunga; mahindi; vibuyu vya asali; nyama ya kuwindwa porini iliyookwa kwenye moto; lebasi; na wakati wa siku kuu kama Milad Nabii, Zumbe akigawa sarafu za fedha, kama Sadaka.
Zumbe Mwinyi Mkuu akiheshimika kama Kiongozi mwenye weledi, huruma, na kujali kaumu aliokuwa akiisimamia.
Siku ya siku, kinyozi alipokwenda kumnyoa nywele Mwinyi Mkuu, na kumpunguza ndevu, siku ya alkhamis kama kawaida, akakuta pameota pembe mbili kwenye kichwa cha Mwinyi Mkuu.
Kinyozi akaendelea na kazi yake, huku akiangalia zile pembe kwenye kichwa cha Zumbe.
Alijikaza, hakusema kitu juu ya pembe zilizoota kwenye kichwa cha Zumbe, lakini tumbo lilianza kuchemka.
Alijikaza, akamaliza hadi kupunguza kucha za Zumbe. Akapewa ujira wake, na haraka, akakimbia kwa mkewe.
Akamwita mkewe kando.
Akamwambia apa kwa jina la Mwenyenzi Mungu kuwa nitakachokwambia, hutomwambia mtu mwingine.
Mke wa kinyozi alipoona mumewe ameshikwa na tumbo la kuharisha, akaapa
“Haki ya Mungu sintomwambia mtu yeyote hiyo siri”.
Ndipo kinyozi kusema kwa mkewe “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe”.
Mkewe kabaki “Khaa….Zumbe ana pembe? Kageuka mnyama?”
Kinyozi wakati huo tumbo limepoa, keshatoa joto tumboni, akamjibu mkewe “Sssh! Usiseme tena”.
Kinyozi akala chakula cha mchana, akenda sokoni ambapo alikuwa na bao la watu wanaonyolewa hukaa. Alipumua vizuri, akaendelea na kazi zake.
Huku nyuma, mke wa kinyozi, tumbo la kuharisha limemkaza. Lazima atoe joto tumboni.
Kila alivyojizuia, tumbo languruma.
Akaenda jirani kwa dada yake na kumwambia “Apa nikikupa siri ya Zumbe Mwinyi Mkuu, hutotoa siri kwa mtu yeyote”.
Dada mtu akaapa “Masahafu ya Mtume sintotoa siri ya Zumbe Mwinyi Mkuu kwa mtu yeyote”.
Mke wa kinyozi akatapika siri ili tumbo lipoe “Kwa taarifa yako, Zumbe kaota pembe..”
Dada yake akauliza “Kaota pembe? Kama za mnyama?”
Mke wa kinyozi akajibu “Si ndiyo, kaota Zumbe Mwinyi Mkuu, na uzumbe wake, na mali zake, na ashraf yake, kumbe ana pembe kwenye kichwa, sijui kama ngiri pori…”
Ooof! Mke wa kinyozi akapumua, keshatua mzigo.
Akarudi kwake.
Huku nyuma, Dada mtu tumbo la kuharisha likamkamata.
Kila anavyojaribu kujizuia, ashindwa. Hana starehe wala jarehe. Tumbo languruma.
Usiku, mumewe aluporudi kutoka mji wa pili, wakati akimtengea chakula, dada wa mke wa kinyozi akamwambia mumewe “Apia kwa mizimu ya kwenu nikikwambia kitu, hutoyasema kwa mtu yeyote mwingine”.
Yule bwana akaapa “Naapa kwa mizimu ya Lango la Mwajeke, sintomwambia mtu kuhusu hiyo siri”.
Ndipo mkewe akasema “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe kichwani, na kwato miguuni”.
Ooof! Tumbo likapoa.
Mumewe hakulala, tumbo la kuharisha lilimkamata.
Alfajiri, akaenda kwa kaka yake, mchanja kuni, akamwambia “Apa kwa jina la Mwenyenzi Mungu kuwa hutomwambia binadamu yeyote, siri nirakayokupa”.
Kaka mtu, mchanja kuni akaapa “Wallah! Billah! Ta’Allah! Sintotoa siri utakayoniambia kwa binadamu yeyote”.
Akaambiwa na nduguye “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe kichwani; kwato badala ya makanyagio; na mkia kama wa wanyani”.
Oooof! Nduguye keshatoa harara tumboni, mwepesiii…
Tumbo la kuharisha likamshika kaka mtu. Kila akiamkiwa “Salaam aleikum” akijibu “Sijui kitu…” huku tumbo lachemka, lazima aharishe.
Siku nzima wakati anauza kuni, akiulizwa bei ya fungu la kuni, ajibu “Sijui kitu…”
Anadhindwa kuharisha ile siri kuhusu Zumbe Mwinyi Mkuu, kwa sababu kaapa kwa Kiapo kikubwa kuliko chote “Wallah! Billah! Ta’Allah!”
Ilipofika jioni baada ya Sala ya La’asiri, tumbo languruma, alishindwa kusali msikitini, kwa mashuzi yaliokuwa yakimtoka.
Akaja tajiri kulipia mzigo wa kuni, mkokoteni mzima, unaoendeshwa na punda wawili.
Jamaa ikabidi aende porini kutafuta kuni.
Tumbo lasokota.
Mwisho, jamaa akaamua kutoa siri kuwa ‘Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; na manyoya mwili mzima’.
Hiyo siri, aliuambia mti mkubwa huku akijifariji kuwa Kiapo chake kilikuwa kutomwambia binadamu, siyo mti.
Ooooooofffff!
Tumbo likapoa.
Akakusanya kuni, akabebesha matenga ya punda, akapeleka mjini.
Mwepesi kabisa.
Wiki haijapita kufikia alkhamis ya pili, walikwenda porini watengeneza ngoma za Kinyamkela.
Wakatafuta mti mzuri wa kutengenezea ngoma, wakaona mti ule, uliovebeshwa zigo la siri kuwa ‘Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; manyonya’.
Wakakuta mti umevimba kati kati, wakajadili, wakaamua huo mti unafaa.
Wakaukata, wakachukua magome kwenda kutengeneza ngoma, zitakazofika 18.
Wakati wanajikusanya, wakaja wanawake wakaomba wachukue vipande vya matawi wakatumie kuni.
Ngoma zikatengenezwa, zikaambwa, jumatano kabla ya alkhamis, pakapigwa ngoma ya tambiko.
Ngoma zikipigwa, zikawa zinasema “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; manyoya…”
Kila ngoma zikipigwa, zinaimba wimbo huo “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; manyoya..”
Huku wale wanawake waliookota kuni pale kwenye mti uliokatwa walipowasha na kukoleza kuni, nazo zikawa zinaimba “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; manyoya…”.
Dah!
Kaumu ya mji mzima ikawa sasa wimbo ni huo “Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; manyoya; na nyeti ya sokwe…”
Taarifa inazunguka mpaka miji ya jirani.
Binadamu wanasema.
Ngoma zinasema.
Kuni zinasema.
Mpaka asubuhi ya alkhamis, kinyozi hakwenda kwa Zumbe Mwinyi Mkuu kumnyoa nywele; kumpunguza ndevu; na kumkata kucha; ili awe nadhifu siku ya Ijumaa.
Mke mdogo wa Zumbe Mwinyi Mkuu ikabidi amwambie Zumbe kuhusu hiyo ‘taarifa’.
Zumbe akaamua kuita kinyozi mwengine, na kunyolewa kati kati ya uwanja wa majalis/mikutano.
Akaagiza wafanyakazi wake wagawe sharubati na halwa.
Akavua baragashia. Watu wamekusanyika!
Kinyozi mgeni akaanza kumnyoa nywele Zumbe Mwinyi Mkuu, akakuta makovu mawili kichwani kwa Zumbe.
Kwa utani, Zumbe Mwinyi Mkuu akasema “niliota majipu, mawili makubwa yalikaa kama pembe. Wake zangu wakanipaka dawa ya halidi/bizari ya njano na asali, majipu yakaiva, wakayatumbua. Sikutaka kumpa taklif kinyozi wangu”.
Sahiba wa Zumbe Mwinyi Mkuu akasogea karibu, akaona makovu ya majipu yaliotumbuliwa na kupona.
Umati uliokusanyika wakaanza kuambaa.
Zumbe Mwinyi Mkuu akawasihi wasiondonke bila kunywa sharubati na kula halwa.
Hiki, ndiyo kisa cha uongo na uzushi na ushenzi unavyotapakazwa!
Iwe fundisho kwetu, lakini binadamu wazito kufata sirat’l mustaqin, njia ya wokofu, na wepesi kuhukumu.
Cha kusikitisha, tuliowakabidhi dhima ya kusimamia ustawi na ulinzi wetu, ndiyo wanakuwa wakwanza kuamini ‘Zumbe Mwinyi Mkuu kaota pembe; kwato; mkia; manyoya; …’ bila kujali hisia za muathirika, wala kufikiria athari atakoyapata mtu.
Hii tabia imejengeka JMT kwetu.
Mungu anatuona.
Leila Sheikh
Tanga,
November 23, 2021
Leave a Reply