Kebehi za maumbile- Fat Shaming
BAADHI yetu tumepitia tashtiti za kebehi juu ya miili yetu.
Kuanzia jinsi tulivyoumbwa; hadi uzito wa miili.
Imekuwa ndiyo utamaduni siku hizi- wanawake, na mara nyingine wanaume, kukebehi miili na maumbile ya wenzao.
Wengi wetu ni wahanga wa kebehi hii.
Waweza kutana na mtu, wala hamfahamiani vizuri, ataanza kukuchambua kuanzia kichwa, hadi nyayo za miguu, kwa kauli yenye maneno ya kubeza, ambayo mara nyingi, huchoma hisia kama msumari wa moto.
Jinsi jamii zetu zilivyo, hatukufundishwa tujibu vipi kebehi hizo.
Wengi wanabaki kuugua kimya kimya.
Wengi zaidi, wanakosa amani, na kupoteza ari ya kujiamini.
Mchezo huu, sijui niite mchezo, wa kuwakandamiza wenzetu, kuwa:
▪︎ Wana shepu mbaya
▪︎ Miguu njukuti
▪︎ Nywele kinyonyoke
▪︎ Mnene kama mbuyu
▪︎ Mweusi kama piko ya nywele
▪︎ Kapauka kama mgonjwa wa safura
▪︎ Kakonda utadhani kijiti cha fagio la cherewa
▪︎ kaumbwa kushoto, kushoto
▪︎ Ana kikwapa
Orodha ni ndefu.
Kwenye hiyo orodha, miye nshaitwa ‘mbuyu’; ‘papai bichi’; baby elephant’.
Sijui wenzangu.
Wapo wanaokusogolea karibu, wanakuangaliaa, afu wanakwambia “Ushaanza kuzeeka” 🤓.
Wakati huo upo kwenye sweet early 50s.
Yaani!
Ikafika wakati, wanaharakati tukaanzisha mafunzo juu ya Taswira ya Miili Yetu au Body Image.
Tulitayarisha nyenzo za kufundishia, mojawapo, ni Body Mapping- Kuchora ramani ya miili yetu. Baada ya kuchora ramani hiyo, tunawauliza washiriki wa mafunzo ‘Kitu kipi kinawavutia kwenye miili yao; na kipi hakiwavutii’.
Baada ya hapo, tunajenga ari ya kujiamini kwa washiriki.
Hizi warsha zimesaidia mno.
Binafsi, japo ni mkufunzi kwenye hizo warsha, nami nikajijengea ari.
Hizi warsha tulifanya kupitia Akina Mama wa Afrika AMWA; TGNP; na YALI.
Dada Hope Chigudu mwanaharakati alikuwa mkufunzi mkuu, mimi msaidizi.
Warsha zilisaidia kujenga umadhubuti miongoni mwa washiriki.
Siku hizi mtu akinikong’ota kwa maneno, ninakuwa mwepesi kumjibu.
Akiniita ‘Mbuyu’, mie namwita ‘Biringanya’.
Nipe Nikupe- Tit for Tat!
Bahati mbaya, warsha aina hizi, za kujenga ari na ukakamavu, hazijaenea hapa JMT.
Ndiyo maana wanawake wanakuwa waathirika wa mabezo; kebehi; tashtiti; na mara nyingine, kuumizwa hisia hadi kulia machozi.
Huu utamaduni upo, na utaendelea kuwepo, iwapo tunakubali kuonewa.
Tujadili
Together We Can Make it Happen
Leave a Reply