Je, Harakati za Ukombozi wa Wanawake Umetengeneza Mashoga?
BAADHI yetu tumekuwa wanaharakati tokea bado tunasoma shule, high school.
Tulivutiwa na ile Dira ya:
▪︎ Haki kwa wote
▪︎ Usawa kwenye fursa za elimu; ajira; biashara; uongozi nk
▪︎ Ukakamavu kwa mabinti na wanawake, tusionewe; tusifanyiwe ngono lazimishi; tusibaguliwe
▪︎ Tupewe stadi za maisha ili tuweze kukabiliana na changamoto
Sisi, wanaharakati wa Afrika, hususan Afrika Mashariki, tulikaa kwa pamoja, na tuliamua kuwa Hatutaki kuwa wanaume; wala hatutaki kuchukua nafasi ya mwanaume kwenye jamii.
Tunachotaka ni:
▪︎ Heshima juu ya utu wetu
▪︎ Fursa bila ubaguzi ili tuweze kujikimu, sisi na familia zetu
▪︎ Vipaji vyetu vitambulike; na michango yetu kwenye maendeleo ya Taifa, ipewe utambuzi.
Hatukutaka kujigeuza majike- dume; la hasha.
Nakumbuka mimi nilikuwa Dogo, nikaandika makala, kwa Kimombo kuwa “We do not want to be caricatures of the male stereotype“.
Tulichotaka, ni kupaza sauti, ili tupewe fursa kwenye kujiendeleza; na tunapofanya hivyo, tunaendeleza familia; jamii; na Taifa.
Tulijitahidi kubaki ndani ya maadili yenye kuleta heshima stahiki kwa wanawake na wanaume.
Iwapo mwanamke amefiwa na mume, na ni single mother/mzazi pekee; au mwanamke ameachika kwa mume ili kulinda afya ya akili; hisia; na kiwiliwili chake, haimaanishi kuwa tunafata mrengo wa Imani kuwa ‘Asasi ya Ndoa Imepitwa na Wakati’, bali tunaamini kuwa ‘Ni vema tukajiweka ba’idi/kando, ili mwenza wetu aweze kupata furaha; na sisi, tupate ahueni‘.
Haimaanishi kuwa tunapinga asasi ya ndoa, bali tunafikiria usalama wa wanandoa. Tusije kunyofoana macho.
Na iwapo wanawake wanaamua kungoja mpaka wapate mwenza mwingine, atakaekuwa na sudi naye ya furaha, haya ni maamuzi binafsi.
Mataifa ya Ulaya na Marekani, ambapo maandiko mengi ya kifeministi yametoka, wanayo mirengo aina kadha, juu ya uanaharakati na utetezi wa haki za wanawake.
Sasa, pamezuka wimbi la ushoga na wanaume kubadili jinsia ili watambulike kama wanawake; na wapo mabinti waliobadili jinsia watambulike kama wanaume.
Je, hii imeletwa na uanaharakati?
Au ni Ule Uhuru Usio na Kanuni; wala Mipaka?
Maana ya Uhuru, siyo kujiachia, bila kuwa na Kanuni na Heshima kwa Uhuru wa wenzetu.
Uhuru lazima uzingatie haki; heshima; uadilifu; na sheria tulizoweka.
Mfano yupo mwanaume mmoja, Data Talks, alinitongoza nikamkataa; akanifanyia kila aina ya uovu.
Ningeweza kumfata ofisini kwake nikamvunja mikono kap kap; kama tunavyovunja vibawa vya kuku.
Sikufanya hivyo, badala yake, nikamrudishia mapigo kama vita ya msituni.
HANIWEZI!
Tunaweza kuwakomesha watesi wetu bila ya kuchukua hatua za kijinai.
Turudi kwa mtambaa wa mitandao ya ushoga.
Je, ni uanaharakati wetu?
Au utandawazi?
Au wazazi na walezi tumejikita kwenye mafanikio ya kifedha, ile “Mimi nina gorofa, wewe Leila unayo nyumba ya Kipemba”.
Au “Naendesha V 8 na Mercedes, wewe Leila wapanda bajaji?”
Tutafakari,
Together, we can make it happen
Leave a Reply