Dondoo Muhimu kusaidia wenye hisia za kujiua

Dondoo Muhimu kusaidia wenye hisia za kujiua

KWANZA kabisa, tuweke bayana yafuatayo:

■ Hapa kwetu JMT, suala la mtu kupitia hisia za kujiua, kwa kuamua kuchukua maisha yake, huwa hatulizungumzii.
Na tunapolijata, ni pale mtu ameshajiua; na mara zote, huwa tunamsema kwa ubaya, huyo mtu aliechukua maisha yake.
Hatuna hisia za huruma kwa mtu anaeamua kujiua.
Inawezekana kutokana na mafundisho ya Imani, kuwa ni dhambi kubwa, kuamua kujiua, na kutimiza tendo la kujiua.
Yapo madhehebu mengine ambayo mtu aliejiua, hapati Sala anapizikwa.
Yapo makabila yanayokataa mtu aina hiyo kuzikwa kwenye makaburi ya familia. Wanaona ni balanzi.

■ Bado hatujaunda vikundi vya kutoa sapoti kwa mwenzetu anaepitia hisia za kutaka kujiua.
Na pia vikundi vya sapoti kwa wazazi; wanafamilia; rafiki; wa mtu aliefariki kwa kujiua.
Jamii inabaki kunyamaza kimya, kama lile tendo la mwenzetu kujiua halikutendeka; au tunasema pembeni, kwa masikitiko; au kwa umbea na lawama.
Hili ni pengo kubwa mno; kukosa vikundi vya sapoti kwa wahanga waliojaribu kujiua; au familia zenye mtu aliejiua.

Iwapo tungekuwa na vikundi vya kutoa sapoti kwa mtu anaepitia hisia za kutaka kujiua; tungeweza kuokoa maisha mara nyingi zaidi.

■ Jamii zetu hatujaweka mfumo wa kusaidia mwanajamii mwenye nia ya kujiua.
Hata kwenye Vyuo Vya Ustawi Jamii, hili somo halifundishwi kwa kina, kwa Maafisa Ustawi Jamii watarajiwa.
Inatubidi kama Taifa, tuliangalie hili, hasa wakati wa kupanga mitala ya mafunzo ya vyuo aina hiyo.

■ Asasi za dini hazijaweka vitengo vya kusaidia watu/waumini, wenye kupitia hisia ya kutaka kujiua.
Inabidi viongozi wa Imani waambiwe juu ya pungufu hili, na hatua stahiki, kuchukuliwa.

■ Hatujaweka laini za simu bila malipo- Hotline, kusaidia wenye kupitia hisia za kutaka kujiua.
Mataifa mengine wameweka mfumo huu kwa kushirikiana na makampuni ya simu.
Na hizi Hotline husaidia mno, kumpa ushauri nasaha mtu anaetaka kujiua.
Mfumo huu inatubidi tuanze kuweka hapa kwetu.
Asasi za kiraia/AZAKI na Jumuiya za Imani, pamoja na makampuni ya simu, wangeunda Jumuiya ya Kusaidia Walengwa/victim na familia zao.

■ Vyombo vya habari vinaweza kusaidia kwa kutoa matangazo ya mara kwa mara, kusaidia wenye nia ya kujiua.

■ Tusichekane, wala tusinyoosheane kidole, iwapo mwenzetu anapitia kipindi cha majonzi, na anafikiria kujiua.
Tusilaumiane iwapo mmoja wetu amepoteza mtoto; au ndugu; au mwanandoa; kwa kujiua.
Hatuwezi kufahamu kinachopita kwenye fikra na hisia za mtu anaeamua kujiua.

■ Tusifanye masikhara endapo mwenzetu anapitia kipindi cha majaribu; au analalamikia ugumu wa maisha; kwa kumwambia “Jiue, kama maisha yamekushinda”.
Ushauri aina hii SIYO utani.
Ni hatari na unaweza kuleta madhara makubwa.

■ Tusiweke sumu majumbani mwetu.
Mfano sumu ya kuua panya; au vifaa vyenye ncha kali; wakati mtoto au ndugu anapitia kipindi cha hisia za kutaka kujiua.
Tena siku zote huwa tunasema wanaouza sumu ya kuua panya, WAKATAZWE. Ipigwe marufuku kabisa.
Yaani sumu inauzwa nje, nje!

■ Shule/Vyuo ziweke Dawati la Kusikiza watoto/vijana, kuwasaidia, wasijekufanya maamuzi ya kujiua.

Muhimu

Tuwasikize wenzetu wanaopitia kipindi kigumu.
Unaweza kuokoa maisha.

 

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *