Matusi ya nguoni

Matusi ya nguoni

WACHACHE miongoni mwa wanajamii wa JMT, wanaelewa kuwa Matusi ya Nguoni ni Kosa la Jinai
Hii imeainishwa kwenye Sheria ya Makosa ya Kujamiiana SOSPA 1998, kwenye Utangulizi, pale ambapo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana SOSPA 1998, imeweka bayana kuwa

SOSPA 1998 ni Sheria inayorekebisha Sheria kadha, juu ya masuala ya jinai ya kingono, ili kulinda heshima; staha; uhuru; usalama wa wanawake na watoto

Hapa wananchi tumewekewa bayana, nia na madhumuni ya kutungwa na kupitisha SOSPA 1998.
Imeainisha jinai za kingono.
Imeweka Vifungu vya adhabu kwa atakayekutwa na hatia ya jinai ya kingono.
Imerekebisha Kanuni za Makosa ya Jinai- Penal Code, ili iweke msisitizo wa adhabu kwa wahalifu wanaotenda jinai ya kingono.

Mara zote, jamii inapoongelea ukatili wa kijinsia, tunachukulia:

■ Kupiga mwanandoa au mpenzi

■ Kubaka

■ Unajisi wa watoto

■ Ukeketaji

■ Kuishi kwa pato litokanalo na biashara ya ngono/Dada Poa; au kuwadi anaeuza wanawake au watoto kwenye biashara haramu ya uuzaji wa binadamu kwa matendo ya ngono

■ Kufanya tendo la ngono, kinyume cha maumbile; baina ya mwanaume na mwanaume, au mwanaume na mwanamke

■ Kuingilia kimwili binti yako; kaka; mjomba; baba mdogo.
Jinai ya incest

■ Ngono lazimishi- Sexual harassment n.k.

Tunasahau jinai moja ambayo hutendeka kila siku; kila dakika; kwenye jamii zetu.
Jinai ya matusi.

Jamii imejenga ganzi juu ya matusi, na wala hatushangai sisi, au mwenzetu akitukanwa.
Mwenendo huu umeweza kujenga hisia kuwa wanawake tunastahili kutukanwa; na hatutakiwi kulalamika.
Unapolalamika, unaonekana kama vile pungueni, akili zimekuruka.
Na mwenendo huu ambao unakubalika kwenye jamii, unakuwa na muendelezo hadi kwenye vipigo; au ubakaji.
Kama jamii, tunashindwa kukemea matusi ya nguoni; udhalilishaji wa mwanamke kwa kumzushia kashfa za kumchafulia hadhi; heshima; staha; na utu wa mwanamke, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Makosa ya Kujamiiana SOSPA 1998.

Hata wanaume wanapotukanana, hutumia maumbile ya faragha ya wanawake, mama zao, kuwatukania.
Hata wanawake wakigombana, hutukanana kwa kutumia msamiati unaohusisha sehemu za faragha za mwili wa mwanamke.

Viongozi wa dini nao hushambulia wanawake, hadi kufikia kuita “Wanawake Najis”.
Najis hiyo ndiyo iliyomtoa huyo Kiongozi wa dini, hadi kusimama juu ya majukwaa na kutusi wanawake.

Mwanamke anapotukanwa matusi ya nguoni, anapata:

▪︎ Fadhaa
▪︎ Madhila
▪︎ Kashfa
▪︎ Aibu
▪︎ Kuchafuliwa hadhi yake
▪︎ Kudhalilishwa utu wake
▪︎ Kuumizwa hisia zake
▪︎ Kuathiri afya yake
▪︎ Kumpa unyonge na kutojiamini
▪︎ Kuminywa uhuru wake wa kuishi kwa furaha na amani

Tatizo, bado hatuainisha kuwa matusi ya nguoni ni ukatili wa kijinsia, ambao inabidi tuupige vita.

Together We Can Make it Happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *