BIMA
TUMEAMBIWA sisi wananchi wa Tanzania kuwa tunaletewa mfumo mpya wa malipo ya tiba; ambao utakuwa kwa mfumo wa Bima ya Afya.
Tumeambiwa kuwa kila mwananchi alievuka umri wa miaka 18, itabidi achangie hiyo ‘Bima ya Afya’.
Hatujaambiwa iwapo wanafunzi waliopo vyuoni ambao wamevuka umri wa miaka 18, nao watalazimika kulipia Bima ya Afya’.
Hatujaelezwa wananchi wa ngazi ya jamii, ambao hutegemea mapato ya msimu mfano wakulima, walime; wavune mazao; watafute masoko ya mazao yao; ndipo wajipatie kipato, wataingizwa vipi kwenye huu mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.
Tukumbuke, kilimo ni kama mchezo wa gudu gudu; wa pata- poteza; kinachotegemea misimu na hali ya tabia nchi.
Aidha masoko nayo ya mazao ya wakulima ni ile “Kuweka mkono gizani“.
Mteja, yaani mnunuzi, mara nyingi ndiye anaepanga bei ya mazao.
Anavyopanga mkulima kwa kufanya tathmini ya uwekezaji aliopandikiza kwenye kilimo; pamoja na nguvu kazi aliotumia, sivyo faida anayopata.
Analima ili aweze kupata senti za kununua bidhaa za madukani.
Chakula chake kinatoka shambani kwake.
Tukiangalia-
▪︎ Mama Lishe
▪︎ Dereva wa boda boda na bajaji
▪︎ Machinga wanaochuuza nyumba kwa nyumba
▪︎ Wachuuzi wa vipodozi
▪︎ Wachuuzi kupitia mitandao
Nk
Orodha ni ndefu, na hawa wote, kipato chao kinakuwa cha msimu.
Na akina yakhe sisi, Wamachinga wa kuuza maneno/seasonal consultants, ndiyo hivyo hivyo.
Je, Wizara imefanya tafiti kuweza kutathmini kama wananchi tutaweza kumudu ulipaji wa Bima ya Afya ya kila mwezi?
Tumezoea kulipia tiba kadri tunavyoumwa.
Hatujazoea kuwekeza kwenye tiba, wakati hatuumwi.
Thuuu!
Mungu apishe mbali.
Ni kama niambiwe niwekeze kwa ajili ya mazishi yangu, ili pawepo na maua; waombelezaji; na biriani.
Mimi nasema “Bima ya Afya itakuwa zigo kwa wananchi”.
Ebu fanyeni tafiti; museme “Ashaakum”; mumlani shetani.
Isijekuwa kibanzi cha mwisho kwenye mgongo wa ngamia, Astaghfirllah.
Together, we can make it happen
Leave a Reply