Utumiaji wa Vipengele vya Sheria

Utumiaji wa Vipengele vya Sheria

KESI za unajisi wa watoto na ubakaji zimekuwepo miaka ya nyuma kabla ya kupitishwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana SOSPA 1998; na hata baada ya kupitisha SOSPA 1998, matukio ya uhalifu wa kingono, yamekuwa yakitendeka.

Sheria tumeletewa kwa ajili ya:

■ Kuwapa adhabu wanaotenda jinai ya kingono/sexual offences.

■ Kupunguza, na hatimaye, kutokomeza kabisa matendo ya jinai ya kingono.

■ Kuweka Misingi ya kuheshimu Hadhi; Heshima; Staha; na Utu wa wanawake na watoto.
Sheria inashinikiza hayo yote- (Preamble to SOSPA 1998).

■ Kupatiwa fidia kwa muathirika wa jinai ya kingono, kupitia mahakama.

■ Kutambua jinai za kingono; na kuainisha jinai za kingono zinajumuisha matendo aina gani, hadi kufikishwa kwenye mahakama.

■ Ni sehemu ya kifuta machozi kwa muathirika wa jinai ya kingono, pale ambapo muhasimu aliemfanyia shambulio la aibu; na kuumiza siyo tu mwili wa muathirika; bali pia hisia za muathirika, na ndugu na marafiki wa muathirika; kuwa haki imetendeka.

■ Kuzuia matukio ya jinai ya kingono yasitokee tena kwenye jamii zetu.

■ Ni Haki yetu kusikizwa na mahakama, ili tutoe machungu tuliopewa na mjinai alietenda jinai ya kingono, dhidi yetu.

SOSPA 1998 ni Sheria ya kimapinduzi, siyo tu Tanzania, bali Bara Afrika; na kwingineko ulimwenguni.
Mifano:

▪︎ SOSPA 1998 imeainisha makosa ya jinai ya kingono, na kuweka Vifungu vya adhabu, kwenye Kanuni za Makosa ya Jinai/Penal Code.

▪︎ Kwa mara ya kwanza, muathirika wa jinai ya kingono, akaanza kutambulika kwenye mchakato wa sheria; kinyume na kabla ya kupitishwa SOSPA 1998, ambapo ilikuwa Jamhuri Dhidi ya Mjinai.
SOSPA 1998 imempa sura na jina muathirika; na yeye, anakuwa mmoja wa washtaki wa malalamishi.
Hii imempa heshima na hadhi muathirika, kuwa yeye ndiye mlalamishi wa kwanza; akisaidia na Jamhuri, kupata haki mahakamani.

▪︎ SOSPA 1998 imeweka Vifungu vya fidia kwa muathirika ili aweze kupata afueni, baada ya kupitia kipindi cha ukatili wa kijinsia.

▪︎ SOSPA 1998 imeainisha na kuharamisha ukeketaji wa mabinti na wanawake.
Jambo ambalo haijawahi kutokea ulimwenguni, hadi kupeleka serikali ya JMT, GoT, kupewa tuzo 9 za Utendaji Bora kutekeleza Haki za Wanawake na Ulinzi wa Watoto.
TAMWA nayo ilipata tuzo kadha kwa kupigania uletwaji wa SOSPA 1998.

Orodha ni ndefu, ambayo itabidi tufanyie kazi na kuweka kumbukumbu mwaka 2023, SOSPA 1998 itakapotimiza miaka 25, wa uwepo wa sheria hii ya kimapinduzi.

Mapungufu

Wanaharakati na Afisa wa Jeshi la Polisi, tumegundua yafuatayo kwenye matumizi ya Sheria ya SOSPA 1998:

● Taifa halikuwekeza vya kutosha kwenye mafunzo kwa polisi wanapokusanya vidhibiti vya jinai ya kingono.

● Taifa hatujawekeza vya kutosha kwenye upimaji wa muathirika wa jinai ya kingono, miongoni mwa madaktari; ili ushahidi ukidhi mahitaji mahakamani wakati kesi inaendeshwa.

● Mahakimu nao walihitaji mafunzo kuweza kutumia SOSPA 1998, bila ya jazba; upendeleo; kutokujali kwa sababu imejengeka kwenye hisia na fikra kuwa Mwanamke kayataka mwenyewe, kuvaa nguo za mbano; hata kuwa mrembo, nalo huchukuliwa kuwa ni chachu kwa mwanaume kupata mfadhaiko, hadi kutenda jinai ya kingono.

● Elimu Jamii haikutolewa vya kutosha, kupitia vyombo vya habari; mitandao ya kijamii; mikusanyiko ya Ibada; nk.
Wengi hawafahamu kumshika shika mwanamke bila ridhaa yake; au kumlamizisha tendo la ngono, ni kosa la jinai.
Orodha ni ndefu.

Tukirudi kwenye uendeshaji mashtaka mahakamani, wanasheria janja wanatumia Sheria kiujanja ujanja, hadi mjinai alietenda jinai ya kingono, akaachiwa huru, bila ya adhabu yoyote.
Hii inavunja moyo kwa muathirika.
Imetokea mara nyingi mno, muathirika anabaki kuugua moyo.

Je, kama Taifa, tunahitaji Marekebisho ya Uendeshaji Mashtaka ya Jinai ya Kingono?

Je, kama Taifa

Inatubidi turudie mijadala juu ya SOSPA 1998, na kuiboresha ili haki itendeke?

Je, kama Taifa,

Inatubidi tuwekeze kwenye Elimu Jamii; Mafunzo kwa Waendesha Mashtaka; Mafunzo kwa Daktari wanaopima na kukusanya ushahidi wa jinai ya kingono?

Je, kama Taifa

Tunahitaji SOSPA 1998 iwepo, wakati wanaharakati tunalumbana. Wapo wanaoita ngono lazimishi Rushwa ya Ngono; na watuhumiwa kupelekwa TAKUKURU. Tupo sisi tunaotaka suala la ngono lazimishi libaki ndani ya SOSPA 1998

Na marekebisho yafanywe kwenye hiyo Sheria ili isotoe mwanya, kwa wajinai kuachiwa bila ya adhabu.

Tujadili..

Together, we can make it happen

Share this post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *